Argentina Yazindua Ndege Maalum Kwa Ajili ya Kombe la Dunia 2026
Kampuni ya ndege ya Aerolíneas Argentinas imezindua ndege mpya maalum itakayotumika kuisafirisha timu ya taifa ya Argentina kuelekea mashindano ya Kombe la Dunia 2026.
Ndege hiyo ya kisasa aina ya Airbus A330-200 imeonyeshwa rasmi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ezeiza nchini Argentina, ikiwa imepambwa kwa rangi zinazofanana na jezi ya timu ya taifa ya nchi hiyo.
Mwili wa ndege umechorwa rangi ya bluu hafifu na nyeupe, huku sehemu ya mkia ikiwekwa namba 10 maarufu inayomheshimu nahodha wa Argentina, Lionel Messi.
Mbali na hilo, injini zote mbili za ndege zimewekwa herufi “C” ikiwa ni ishara ya “Captain” yaani nahodha, jambo lililotafsiriwa na mashabiki wengi kuwa heshima ya kipekee kwa Messi ambaye ameiongoza Argentina katika mafanikio makubwa ya soka duniani.
Sehemu ya chini ya ndege hiyo pia imechorwa nyota tatu za dhahabu, zinazowakilisha mataji matatu ya Kombe la Dunia yaliyowahi kushindwa na Argentina katika historia yake ya soka.
Ndege hiyo itakuwa usafiri rasmi wa timu ya taifa ya Argentina kuelekea na wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia 2026 yatakayoanza rasmi Juni 11, 2026.
Mashindano hayo makubwa yataandaliwa kwa pamoja na nchi za Mexico, Marekani pamoja na Canada, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Kombe la Dunia kuchezwa katika mataifa matatu tofauti kwa pamoja.




Post a Comment
Related Discussions...