Author Avatar
Author: Jina la Mwandishi

Watu zaidi ya 90 wafariki katika mlipuko wa mgodi wa makaa ya mawe China

Watu wasiopungua 90 wamefariki dunia huku wengine wengi wakihofiwa kukwama baada ya kutokea mlipuko mkubwa wa gesi katika mgodi wa makaa ya mawe uliopo kaskazini mwa China.

Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 1:29 usiku wa Ijumaa, Mei 22, katika mgodi wa Liushenyu uliopo mkoa wa Shanxi, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya China, Xinhua.

Ripoti zinaeleza kuwa jumla ya wafanyakazi 247 walikuwa chini ya ardhi wakati mlipuko huo ulipotokea. Mpaka sasa, watu 90 wamethibitishwa kufariki huku wengine 123 wakipelekwa hospitalini kwa matibabu, ambapo wanne wako katika hali mbaya.

Vyombo vya habari vya serikali kupitia CCTV vilisema kuwa zaidi ya wahudumu 755 wa uokoaji na afya wametumwa eneo la tukio huku operesheni za kutafuta manusura zikiendelea.

Ajali hiyo imetajwa kuwa mbaya zaidi katika sekta ya migodi nchini China tangu mwaka 2009, ambapo watu 108 walifariki katika mlipuko mwingine wa mgodi uliotokea mkoa wa Heilongjiang.

Mmoja wa manusura wa ajali hiyo, Wang Yong, aliliambia shirika la CCTV kuwa aliona moshi mkubwa na kunusa harufu ya salfa kabla ya kupoteza fahamu.

“Niliona watu wakikosa hewa kutokana na moshi. Nililala chini kwa karibu saa moja kabla ya kuzinduka mwenyewe. Kisha nikawaita watu waliokuwa karibu nami tukatoka nje ya mgodi pamoja,” alisema Wang Yong.

Video zilizooneshwa na CCTV zilionesha waokoaji waliovaa helmeti wakibeba machela huku magari ya wagonjwa yakionekana eneo hilo.

Rais wa China, Xi Jinping, ameagiza kufanyika kwa juhudi zote kuhakikisha majeruhi wanapatiwa matibabu haraka pamoja na uchunguzi wa kina kuhusu chanzo cha ajali hiyo.

Pia amesisitiza mamlaka zote nchini humo kujifunza kutokana na tukio hilo na kuongeza umakini katika masuala ya usalama mahali pa kazi ili kuzuia majanga makubwa yajayo.

Kwa mujibu wa Xinhua, mmoja wa viongozi wanaohusishwa na kampuni inayomiliki mgodi huo amewekwa chini ya ulinzi wa sheria wakati uchunguzi ukiendelea.

...See more

DISCUSSIONS BOX(MAONI)|REPLY

Related Discussions...