Sarah aeleza jinsi ambavyo alianza kuona dalili za Ugonjwa wa Mpox
Ni Sarah huyu, mmoja wa waathiriwa wa ugonjwa huo katika kaunti ya Mombasa nchini Kenya. Maambukizi ya ugonjwa wa mpox kutokana na aina ya virusi vya monkeypox yalizikumba nchi nyingi barani Afrika. Sara anaeleza dalili za MPOX alipoanza kuugua, anasema,
"Mimi nilianza tu kusikia muwasho baada ya siku mbili nikaona vidonda vimetoka vinatoa maji. Vilianza kutoka kichwani halafu vikafura kwenye shingo, nisingeweza kugeuza shingo, hivyo nikaona vidonda vinazidi kuongezeka. Ndipo nikachukua hatua ya kwenda hospitalini, nikaangaliwe shida nini na baada ya hapo walipata kuwa ni MPOX na hapo nikapewa matibabu."
Na ndipo safari ya Sara kuelekea hospitalini. Alipofika hospitali, alilazwa katika wodi moja iliyoko katika kitua cha kutenga kwa ajili ya wagonjwa wa MPOX, anasema..
“Baada ya kufikishwa pale hospitalini. Tuliwekwa kwa wodi ya wagonjwa wenye MPOX kwa ajili ya matibabu. Nilikaa kwa muda wa wiki mbili nikifuata masharti ya daktari na kusafisha na maji ya moto na chumvi. Halafu unapaka dawa uliyopewa ya maji y, na baada ya hapo unameza vidonge vya maumivu. Madaktari wenyewe walikuwa wanakuja wanatuongelesha wakituambia tusiwe na wasiwasi hapa tumekuja mahali sawa.”
UNICEF na huduma za Umoja wa Mataifa za maji na usafi wa mazingira, WASH imewasaidia kuunga mkono Idara ya Afya ya Kaunti ya Mombasa na kwa kushirikiana na Serikali ya Kenya waliweza kujenga uwezo wa wahudumu wa afya na wahamasishaji wa afya ya jamii, wakiwafundisha kuhusu ugonjwa wa MPOX. Dkt. Mohammed Halif ambaye ni Mkurugenzi wa Kaunti ya Mombasa,Huduma za Kliniki za Afya, anasema
“Tangu kulipomgundua mgonjwa wa kwanza, tulianzisha mara moja vituo vya uendeshaji wa dharura za afya ya umma kuhusu usafi wa mazingira na kujisafi, na ninaona imekuwa ni jambo la ukarimu sana kwa UNICEF kuja na kutoa vifaa vya kunawia mikono ambavyo tumevigawa katika wanajamii.”
Sarah baada ya kutibiwa, akapatiwa ushauri ya jinsi ya kutangamana na wengine.
“Tuliambiwa kwamba ukishatoka nje mwepukane na mambo ya ngono sana na pili mambo ya kushikana shikana. Vile nilitoka hospitalini, nilipewa mtungi wa maji na sabuni mche mzima nikaambiwa Mtungi utakuwa wakuchotea maji toka mtoni na kuoga mzuri, usafi uendelee.”
UNICEF imeendelea kuunga mkono hospitali na pia kufanya uhamasishaji ndani ya jamii ili kuhakikisha kwamba visa vitakavyotokea siku za usoni vitashughulikiwa kwa wakati.
Sarah anatamatisha na furaha akisema familia yake pia wamejawa na furaha baada ya kupona, anasema…
“Niliporudi nyumbani watoto walifurahi sana kuniona. Saa hii nafurahia sana, nashukuru napata usingizi, nalala na najihisi niko sawa zaidi sina yale maumivu nilikuwa nayo.”









image quote pre code