Aliyekuwa Malkia wa Denmark Akimbizwa Hospitalini Baada ya Kupata Mshtuko wa Moyo

Aliyekuwa Malkia wa Denmark, Queen Margrethe II, amelazwa hospitalini baada ya kupata mshtuko wa moyo, jambo lililoleta taharuki kubwa nchini humo na miongoni mwa wafuasi wa familia ya kifalme duniani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na familia ya kifalme ya Denmark, malkia huyo mwenye umri wa miaka 86 alikimbizwa katika hospitali ya Rigshospitalet siku ya Alhamisi, Mei 14, kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya haraka na uchunguzi zaidi.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Malkia Margrethe ataendelea kubaki hospitalini hadi mwishoni mwa wiki huku madaktari wakifuatilia hali yake kwa karibu. Familia ya kifalme ilisema kuwa licha ya uchovu alioupata baada ya tukio hilo, bado anaonekana kuwa na hali nzuri ya kisaikolojia na anaendelea vizuri chini ya uangalizi wa madaktari.

Queen Margrethe II anatajwa kuwa mmoja wa watawala waliodumu zaidi barani Ulaya. Aliiongoza Denmark kwa zaidi ya miaka 52 kabla ya kuamua kuachia rasmi kiti cha enzi mwaka 2024, hatua iliyowashangaza wengi kwani alikuwa mtawala wa kwanza wa Denmark kujiuzulu kwa hiari katika kipindi cha karibu miaka 900.

Katika hotuba yake ya mwisho ya mwaka 2023, Margrethe aliweka wazi kuwa changamoto za kiafya zilichangia uamuzi wake wa kuachia madaraka. Alifichua kuwa alikuwa amefanyiwa upasuaji mkubwa wa mgongo, jambo lililomfanya kutafakari kuhusu mustakabali wa familia ya kifalme na umuhimu wa kuandaa kizazi kijacho kuongoza taifa hilo.

Baada ya kuondoka madarakani, alimkabidhi mwanawe, King Frederik X, jukumu la kuongoza ufalme wa Denmark akiwa pamoja na mkewe, Queen Mary, ambaye alizaliwa nchini Australia.

Hata hivyo, licha ya kung’atuka, Margrethe aliendelea kubeba hadhi ya “Queen” na kushiriki baadhi ya shughuli rasmi za kifalme. Katika miezi ya hivi karibuni, afya yake imekuwa ikitajwa mara kwa mara baada ya kulazwa hospitalini katika matukio tofauti, ikiwemo baada ya kuanguka katika makazi yake ya Fredensborg Palace.

Wananchi wa Denmark pamoja na viongozi mbalimbali duniani wameendelea kutuma salamu za pole na kumuombea apone haraka huku familia ya kifalme ikiahidi kutoa taarifa zaidi kuhusu maendeleo ya afya yake siku zijazo.

...See more

DISCUSSIONS BOX(MAONI)|REPLY

Related Discussions...