Baharia wa Kitanzania amepoteza maisha  mlango bahari wa Hormuz

Baharia wa Kitanzania amepoteza maisha wakati akihudumu katika meli ya kuvuta iitwayo VOLANS, Shirika la uwakala wa Meli Tanzania, TASAC limeeleza.

Kifo cha baharia huyo kwa jina Mchama Maregesi Mongu, kilitokea tarehe 3 mwezi Mei mwaka 2026.

Meli hiyo iliyobeba bandera ya Umoja wa Falme za Kiarabu, ilikuwa safarini kutokea UAE kuelekea nchini Oman.

Chombo hicho kilishambuliwa na bomu wakati kikivuka kwenye mlango bahari wa Hormuz uliopo kati ya nchi za Iran na Oman.

Katika taarifa yake, TASAC imesema kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zinafuatilia kwa karibu taarifa za tukio hilo ili waweze kuurudisha mwili wa marehemu nchini Tanzania, mara tu utakapopatikana.

''TASAC inaungana na IMO kusisitiza umuhimu wa kulinda maisha ya mabaharia wanapokuwa baharini, hususani katika maeneo yanayohusisha haki ya kupita kwa amani kama inavyolindwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa sheria ya bahari'' Ilisema taarifa hiyo. Via BBC.

WEKA COMMENT HAPA(Reply)

"Karibu kutoa maoni yako. Kumbuka: Link zote za matangazo haziruhusiwi na zitafutwa kiotomatiki".