Daktari Aliyemtoa Mgonjwa Kiungo Kisicho Sahihi na Kusababisha Kifo afunguka!
Daktari mmoja nchini Marekani anayekabiliwa na mashtaka ya kusababisha kifo cha mgonjwa baada ya kuondoa kiungo kisicho sahihi mwilini ametoa maelezo yaliyozua mjadala mkubwa kuhusu tukio hilo la kusikitisha.
Dk. Thomas Shaknovsky kutoka jimbo la Florida anadaiwa kumfanyia upasuaji mgonjwa mwenye umri wa miaka 70 aitwaye William Bryan lakini badala ya kuondoa wengu, aliondoa ini kwa makosa hali iliyosababisha mgonjwa huyo kupoteza damu nyingi na kufariki dunia.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na NBC News, daktari huyo alisema wakati wa upasuaji huo kulikuwa na changamoto kubwa kutokana na damu nyingi tumboni mwa mgonjwa pamoja na utumbo uliokuwa umevimba uliomzuia kuona vizuri eneo lililokuwa linavuja damu.
Katika ushahidi wake chini ya kiapo uliotolewa mwezi Novemba, Shaknovsky alikiri kuwa alikuwa katika hali ya mshtuko mkubwa wakati wa tukio hilo kiasi kwamba alishindwa kutofautisha kati ya ini na wengu.
“Nilikua nimechanganyikiwa sana na nilipoteza utulivu baada ya hali ya mgonjwa kuwa mbaya mezani,” alieleza.
Daktari huyo pia alisema tukio hilo limeacha maumivu makubwa ya kihisia ambayo yataendelea kumtesa maisha yake yote.
Mke wa marehemu, Beverly Bryan, amefungua kesi dhidi ya hospitali na daktari huyo akidai uzembe wa kitabibu na kusababisha kifo cha mume wake. Alisema yeye na mumewe walikuwa safarini Florida kabla ya William Bryan kupelekwa hospitalini kutokana na maumivu ya tumbo.
Kesi hiyo inaeleza kuwa madaktari walimshawishi marehemu kufanyiwa upasuaji wa kuondoa wengu kutokana na tatizo lililokuwa limeonekana katika kiungo hicho. Hata hivyo, wakati wa upasuaji huo, ini liliondolewa badala ya wengu jambo lililosababisha upotevu mkubwa wa damu na hatimaye kifo.
Mahakama pia imeelezwa kuwa baada ya upasuaji huo, kiungo kilichoondolewa kiliandikwa kimakosa kuwa ni wengu ili kuficha kilichotokea.
Mamlaka nchini Marekani zimedai kuwa daktari huyo alifanya makosa kadhaa makubwa wakati wa upasuaji, ikiwemo kubadili aina ya upasuaji na kushindwa kuomba msaada wa madaktari wengine wakati hali ya mgonjwa ilipozidi kuwa mbaya.
Dk. Shaknovsky tayari amepokonywa leseni yake ya udaktari na mwezi uliopita alikamatwa akiwa anafanya kazi ya udereva wa Lyft. Anakabiliwa na shtaka la kuua bila kukusudia ambalo linaweza kumpeleka gerezani hadi miaka 15 endapo atapatikana na hatia.





Post a Comment
"Karibu kutoa maoni yako. Kumbuka: Link zote za matangazo haziruhusiwi na zitafutwa kiotomatiki".