Daktari mmoja kutoka Marekani aliyekuwa abiria wa meli ya kitalii ya MV Hondius, ametoka katika kitengo maalum cha uangalizi wa magonjwa hatari
Daktari mmoja kutoka Marekani aliyekuwa abiria wa meli ya kitalii ya MV Hondius, Dk. Stephen Kornfeld, ametoka katika kitengo maalum cha uangalizi wa magonjwa hatari nchini Marekani baada ya vipimo vipya kuonyesha kuwa hana maambukizi ya hantavirus.
Dk. Kornfeld mwenye umri wa miaka 69, ambaye ni daktari bingwa wa saratani kutoka Oregon, alikuwa amewekwa chini ya uangalizi mkali baada ya vipimo vya awali kuonyesha matokeo yaliyodaiwa kuwa “faintly positive” yaani dalili hafifu za uwepo wa virusi hivyo hatari.
Akizungumza na CNN, Kornfeld alisema alipokuwa ndani ya meli hiyo alisaidia kuwahudumia baadhi ya abiria waliokuwa wameugua, huku naye mwenyewe akipata dalili zinazofanana na mafua.
“Wakati huo tulidhani ni virusi vya kawaida tu. Lakini sasa kuna maswali kama huenda ilikuwa hantavirus, ingawa hakuna uhakika,” alisema.
Kutokana na matokeo hayo ya awali, Kornfeld alipelekwa katika kitengo maalum cha biocontainment katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Nebraska (University of Nebraska Medical Center), ambako wagonjwa wa magonjwa ya kuambukiza hatari huwekwa chini ya uangalizi maalum.
Hata hivyo, vipimo vya kina vya PCR vilivyofanyika baadaye vilionyesha hana hantavirus. Vipimo vya damu bado vinaendelea kufanyiwa uchunguzi zaidi.
Kwa sasa, Kornfeld amehamishiwa katika eneo la karantini pamoja na Wamarekani wengine 15 waliokuwa ndani ya meli hiyo ya MV Hondius. Taarifa zinaeleza kuwa hakuna hata mmoja kati yao anayeripoti dalili za ugonjwa kwa sasa.
Abiria wengine wawili kutoka meli hiyo wanaendelea kufuatiliwa katika Chuo Kikuu cha Emory mjini Atlanta, Marekani.
Hantavirus ni ugonjwa adimu lakini hatari unaoweza kuambukizwa kupitia panya au kinyesi chake, na unaweza kusababisha matatizo makubwa ya mfumo wa upumuaji.





Post a Comment
Karibu Afyaclass Bongo Social,Share mawazo yako hapa au chochote kuhusiana na Makala husika,Karibu Sana Mdau Wetu Muhimu.