Kesi Mbili za Hantavirus Zathibitishwa Katika Meli ya Kitalii – WHO

Shirika la Afya Duniani limethibitisha kuwepo kwa maambukizi ya virusi vya Hantavirus miongoni mwa abiria waliokuwa ndani ya meli ya kitalii iliyokwama karibu na visiwa vya Cape Verde, huku vifo kadhaa vikihusishwa na mlipuko huo.

Kwa mujibu wa shirika hilo, kesi mbili zimethibitishwa maabara, huku nyingine tano zikihisiwa, na kufanya jumla ya visa saba vilivyobainika hadi sasa, ikiwemo vifo vitatu. Taarifa iliyotolewa inaeleza kuwa hadi Mei 4, 2026, watu saba walikuwa wamegundulika kuambukizwa, ambapo mmoja yuko katika hali mahututi na wengine watatu wana dalili za kiwango cha chini.

Mlipuko huo ulitokea ndani ya meli ijulikanayo kama MV Hondius, inayomilikiwa na kampuni ya Oceanwide Expeditions, ambayo ilikuwa safarini kutoka Ushuaia nchini Argentina kuelekea Cape Verde. Maafisa wa afya wameeleza kuwa dalili zilizoripotiwa kwa waathirika ni pamoja na homa, matatizo ya mfumo wa chakula, na kuongezeka kwa kasi kwa matatizo makubwa ya mfumo wa upumuaji.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, ugonjwa huo umeonekana kuwa na mabadiliko ya haraka kutoka dalili za kawaida hadi hali mbaya zaidi kama nimonia, kushindwa kwa mfumo wa upumuaji na mshtuko wa mwili. Shirika hilo linaendelea na uchunguzi zaidi ili kubaini chanzo na ukubwa wa maambukizi hayo.

Aidha, juhudi zinaendelea kuwatafuta abiria wote walioweza kuwa wameathirika, hasa waliokuwa kwenye safari ya ndege ya Aprili 25 kati ya Saint Helena na Johannesburg, ambapo mmoja wa waathirika aliyefariki alisafiri. Inadaiwa kuwa mgonjwa huyo alizidiwa akiwa safarini na baadaye alifariki alipowasili.

Meli hiyo ilikuwa na abiria 147 kutoka mataifa 23 tofauti, yakiwemo Uingereza, Hispania na Marekani. Kwa sasa, abiria mmoja raia wa Uingereza anaendelea kupatiwa matibabu katika chumba cha wagonjwa mahututi jijini Johannesburg, huku wafanyakazi wawili wa meli wakihitaji msaada wa haraka wa kitabibu.

Licha ya uzito wa tukio hilo, Shirika la Afya Duniani limesema kuwa hatari ya ugonjwa huo kuenea kwa kiwango cha kimataifa bado ni ndogo. Ugonjwa wa Hantavirus huambukizwa zaidi kupitia kugusana na panya au kinyesi chao, ingawa katika matukio machache, maambukizi kutoka mtu mmoja kwenda mwingine yamewahi kuripotiwa.

Shirika hilo limeeleza kuwa litaendelea kufuatilia kwa karibu hali hiyo huku likiendelea na uchunguzi zaidi ili kudhibiti na kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

WEKA COMMENT HAPA(Reply)

WEKA MAONI HAPA(Reply)