Kichwa cha marehemu James Temba, mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kimepatikana

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limethibitisha kupatikana kwa kichwa cha marehemu James Temba, mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), siku sita baada ya kuzikwa kwa mwili wake uliokuwa hauna kichwa.

Kichwa hicho kimepatikana katika eneo la Kitunda Kibeberu, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, kikiwa kimefukiwa ardhini. Polisi wameeleza kuwa mabaki hayo yalikutwa baada ya kuendelea kwa uchunguzi wa tukio hilo lililoibua taharuki kubwa kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumatano Mei 13, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema jumla ya watuhumiwa watano wanashikiliwa kuhusiana na mauaji hayo.

Amesema mbali na watuhumiwa waliotajwa awali, polisi wamemkamata pia Said Ally maarufu “Side”, mwenye umri wa miaka 31, anayetajwa kuwa mganga wa kienyeji.

“Sehemu ya kichwa hiki kimekutwa kimefukiwa ardhini na waliotekeleza uhalifu ule. Jumla ya watuhumiwa watano wanashikiliwa, akiwemo mtu mwingine aliyefahamika kwa jina la Said Ally maarufu Side ambaye ni mganga wa kienyeji,” amesema Kamanda Muliro.

Aidha, amesema taratibu za kisheria zinaendelea kukamilishwa ili mamlaka husika ziendelee na hatua nyingine za uchunguzi pamoja na sheria dhidi ya watuhumiwa hao.

Kwa upande wake, baba mzazi wa marehemu, Rogers Temba, amesema licha ya kuwa bado yupo Moshi mkoani Kilimanjaro, tayari amepokea taarifa za awali kuhusu kupatikana kwa kichwa hicho.

“Wamekipata katika eneo la Kitunda Kibeberu, lakini polisi bado wanaendelea na kazi yao,” amesema Rogers kupitia mazungumzo ya simu. via globalpublishers.

...See more

Related Discussions...

WEKA COMMENT HAPA(Reply)

Karibu Afyaclass Bongo Social,Share mawazo yako hapa au chochote kuhusiana na Makala husika,Karibu Sana Mdau Wetu Muhimu.