Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara,Yanga wapigwa Faini ya Milioni 30
Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga maarufu kama Young Africans, wamekumbana na adhabu nzito kutoka Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kufuatia matukio yaliyojitokeza kwenye mchezo wa dabi dhidi ya Simba uliochezwa Mei 3, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB, Yanga imetozwa faini ya Shilingi milioni 30 baada ya wachezaji pamoja na maofisa wa benchi la ufundi kukataa kutumia vyumba rasmi vya kubadilishia nguo vilivyopo ndani ya Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Stadium. Badala yake, timu hiyo ilidaiwa kutumia nyumba iliyopo nje ya uwanja huo, upande wa pili wa barabara, jambo lililotajwa kuwa ni kinyume cha kanuni za ligi.
Mchezo huo mkubwa wa Kariakoo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2 uliibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka nchini, huku matukio ya ndani na nje ya uwanja yakivuta hisia za wengi zaidi kuliko matokeo yenyewe.
Mbali na faini hiyo, kamati hiyo pia imeitoa onyo kali kwa Yanga kutokana na kuchelewa kufika uwanjani siku ya mchezo. Kwa mujibu wa ratiba rasmi ya ligi, timu ilitakiwa kuwasili saa 10:30 alasiri lakini ikawasili dakika tano baadaye, saa 10:35 alasiri.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Yanga, Walter Harson, amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Shilingi milioni moja baada ya kupatikana na hatia ya kumsukuma kiungo wa Simba, Clatous Chama, wakati wa mchezo huo wenye ushindani mkubwa.
Adhabu hizo zimeendelea kuonyesha msimamo mkali wa mamlaka za soka nchini katika kuhakikisha nidhamu, utii wa kanuni na usalama vinazingatiwa katika michezo ya ligi kuu, hasa kwenye mechi zenye ushindani mkubwa kama Dabi ya Kariakoo.





Post a Comment
"Karibu kutoa maoni yako. Kumbuka: Link zote za matangazo haziruhusiwi na zitafutwa kiotomatiki".