Mchezaji wa zamani wa klabu ya Arsenal, Lucas Torreira, ameripotiwa kushambuliwa chanzo wivu wa kimapenzi.

Mchezaji wa zamani wa klabu ya Arsenal, Lucas Torreira, ameripotiwa kushambuliwa akiwa kwenye shughuli za ununuzi mjini Istanbul nchini Uturuki, katika tukio linalodaiwa kuchochewa na wivu wa kimapenzi.

Kiungo huyo wa Galatasaray mwenye umri wa miaka 30, alishambuliwa nje ya mgahawa mmoja katika eneo la Beyoglu siku ya Jumanne, Mei 12, baada ya kupiga picha na mashabiki waliokuwa wamemzunguka.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kwa polisi, Torreira alisema mwanamume mmoja alimfuata akitaka kupiga picha naye kama mashabiki wengine walivyokuwa wakifanya. Hata hivyo, muda mfupi baadaye, mtu mwingine alimkaribia ghafla na kumpiga ngumi upande wa kushoto wa kichwa chake.

Torreira alisema hakuelewa kilichokuwa kinaendelea mara baada ya kushambuliwa, na ndipo dereva wake pamoja na rafiki yake waliokuwa karibu waliingilia kati ili kumuokoa na kumtenganisha na mshambuliaji huyo.

“Nilijaribu kujilinda, na dereva wangu pamoja na rafiki yangu walinisaidia kumzuia mtu huyo. Baada ya kutenganishwa, alikimbilia kwenye teksi akitaka kuondoka eneo hilo,” Torreira alinukuliwa akieleza polisi.

Baada ya tukio hilo, mchezaji huyo alienda hospitalini kufanyiwa uchunguzi ambapo madaktari walibaini kuwa alikuwa na wekundu kati ya jicho lake la kushoto na nyusi kutokana na kipigo hicho. Pia alieleza kuwa alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya kichwa.

Torreira amesema hajawahi kumuona mshambuliaji huyo hapo kabla na hajui sababu iliyomfanya kufanya shambulio hilo. Amefungua rasmi malalamiko dhidi ya mtuhumiwa huyo na kusisitiza kuwa anataka hatua za kisheria zichukuliwe.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uturuki, mtuhumiwa huyo aliyefahamika kwa herufi za mwanzo YY alikuwa tayari amewahi kuwekewa zuio la kutomsogelea mpenzi wa Torreira kutokana na madai ya kumsumbua. Aidha, anaripotiwa kuwa na rekodi ya kosa la kusababisha majeraha kwa makusudi.

Ripoti zaidi zimeeleza kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akitoa vitisho dhidi ya Torreira kupitia mitandao ya kijamii, huku chanzo kikidai kuwa alikuwa na wivu kuhusu uhusiano wa kimapenzi wa nyota huyo wa Galatasaray.

...See more

Related Discussions...

WEKA COMMENT HAPA(Reply)

Karibu Afyaclass Bongo Social,Share mawazo yako hapa au chochote kuhusiana na Makala husika,Karibu Sana Mdau Wetu Muhimu.