Mvutano wa Marekani na Iran, Jeshi la Marekani limetangaza meli zake mbili kupita Salama Mlango wa Hormuz
Jeshi la Marekani limetangaza kuwa meli mbili za kibiashara zenye bendera ya Marekani zimefanikiwa kuvuka njia muhimu ya baharini ya Strait of Hormuz, hatua inayotafsiriwa kama mwanzo wa jitihada za kufungua tena njia hiyo iliyokuwa imefungwa kwa muda kutokana na mvutano wa kijeshi kati ya Marekani na Iran.
Hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa Project Freedom uliotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump, unaolenga kurejesha usafiri wa biashara katika njia hiyo nyeti inayotumiwa kusafirisha mafuta na bidhaa muhimu duniani.
Kwa mujibu wa United States Central Command (CENTCOM), meli hizo zilipatiwa ulinzi na manowari za kivita za Marekani wakati wa safari yao katika Ghuba ya Uajemi. Ulinzi huo umewekwa ili kuhakikisha usalama wa vyombo vya usafiri kufuatia vitisho vinavyotolewa na Iran.
Hata hivyo, hali imeendelea kuwa tete baada ya jeshi la Iran kuonya vikosi vya Marekani visiingie katika njia hiyo, likisisitiza kuwa meli zote za kibiashara zinapaswa kuratibu safari zao kupitia mamlaka za Iran.
Katika tukio lingine lililoongeza mvutano, Kamanda wa kijeshi wa Marekani, Brad Cooper, alieleza kuwa helikopta za kijeshi za Marekani zilizamisha boti ndogo sita za Iran zilizokuwa zikilenga kushambulia meli za kiraia.
Wakati huohuo, Iran kupitia shirika lake la habari la Fars News Agency ilidai kuwa imefanikiwa kushambulia manowari ya Marekani kwa makombora mawili karibu na eneo la Jask. Hata hivyo, Marekani imekanusha vikali madai hayo na kusisitiza kuwa hakuna meli yake iliyopigwa.
Mvutano huo pia umeathiri nchi jirani, ambapo United Arab Emirates imelaani kile ilichokiita uchokozi wa Iran baada ya droni ya Iran kusababisha moto katika kituo cha mafuta cha Fujairah. Tukio hilo liliwajeruhi watu watatu na kuibua tahadhari ya makombora mara tatu ndani ya siku moja ikiwa ni mara ya kwanza tangu makubaliano ya kusitisha mapigano kuanza.
Aidha, taarifa kutoka jeshi la Uingereza zilieleza kuwa kulikuwa na meli ya mizigo iliyokuwa ikiteketea kwa moto karibu na pwani ya UAE, tukio linaloonyesha kuongezeka kwa hatari katika eneo hilo.
Licha ya mafanikio ya kupita kwa meli hizo mbili, bado kuna wasiwasi mkubwa kuhusu iwapo kampuni nyingi za usafirishaji na bima zitakuwa tayari kuendelea kutumia njia hiyo. Iran imeendelea kusisitiza kuwa itachukua hatua dhidi ya vyombo vyovyote vinavyopita bila idhini yake.
Kwa ujumla, hali ya usalama katika Strait of Hormuz bado ni ya wasiwasi mkubwa, huku dunia ikifuatilia kwa karibu hatua zinazochukuliwa na pande zote mbili katika kuzuia mgogoro mkubwa zaidi wa kijeshi.





Post a Comment
WEKA MAONI HAPA(Reply)