Ndege yaangukia nyumba Watu wawili wamepoteza maisha

Watu wawili wamepoteza maisha baada ya ndege ndogo aina ya Piper PA-28 kuanguka kwenye nyumba katika mji wa Akron, Jimbo la Ohio nchini Marekani, tukio lililosababisha moto mkubwa na taharuki kwa wakazi wa eneo hilo.

Ajali hiyo ilitokea Alhamisi Mei 14, 2026 muda mfupi baada ya ndege hiyo kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Akron Fulton uliopo karibu na eneo la tukio. Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka mamlaka za zimamoto, ndege hiyo ilianguka moja kwa moja kwenye nyumba ya makazi na kusababisha mlipuko mkubwa ulioteketeza sehemu ya nyumba hiyo kwa moto mkali.

Idara ya Zimamoto ya Akron imethibitisha kuwa watu wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo walifariki dunia papo hapo kutokana na athari za ajali hiyo. Hata hivyo, hakuna mkazi wa nyumba iliyogongwa aliyeripotiwa kujeruhiwa, jambo ambalo limeelezwa kuwa ni bahati kubwa kutokana na ukubwa wa moto uliotokea.

Mashuhuda wa tukio walisema waliona moshi mzito ukifuka angani na kusikia mlipuko mkubwa kabla ya vikosi vya uokoaji kufika eneo hilo. Baadhi ya wakazi wa nyumba za jirani waliondolewa kwa muda kama tahadhari ya usalama wakati shughuli za kuzima moto zikiendelea.

Mkuu wa Idara ya Zimamoto ya Akron, Sierjie Lash, amesema walipokea simu nyingi kutoka kwa wananchi waliokuwa wakiripoti kusikia milipuko na kuona moto mkubwa katika eneo hilo. Vikosi vya zimamoto vilifika haraka lakini vilikuta nyumba ikiwa tayari imeathirika vibaya na moto uliokuwa ukiendelea kusambaa.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA) pamoja na Bodi ya Taifa ya Usalama wa Usafiri (NTSB) zimeanza uchunguzi maalum ili kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo. Hadi sasa, majina ya watu waliopoteza maisha bado hayajatangazwa rasmi huku uchunguzi ukiendelea.

Tukio hilo limezua huzuni kubwa miongoni mwa wakazi wa Akron, huku wengi wakieleza kushtushwa na namna ajali hiyo ilivyotokea ghafla katika eneo la makazi ya watu.

...See more

DISCUSSIONS BOX(MAONI)|REPLY

Related Discussions...