Rais wa Zamani wa Botswana Festus Mogae Afariki Dunia Akiwa na Miaka 86
Rais wa zamani wa Botswana, Festus Mogae, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 86, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rais wa sasa wa nchi hiyo, Duma Boko.
Kupitia taarifa yake, Boko amesema Botswana imepoteza kiongozi muhimu aliyelitumikia taifa kwa moyo wa uzalendo na kujitolea kwa miaka mingi.
“Leo Botswana inaomboleza mwanasiasa na mzalendo mashuhuri ambaye maisha yake yote aliyatoa kwa ajili ya kulitumikia taifa lake,” alisema Boko akitangaza kifo hicho kilichotokea mapema Ijumaa.
Mogae aliiongoza Botswana kuanzia mwaka 1998 hadi 2008 na anatajwa kuwa mmoja wa viongozi waliochangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa uchumi na mifumo ya utawala nchini humo katika kipindi cha ukuaji mkubwa wa mapato yatokanayo na madini ya almasi.
Kwa muda mrefu kabla ya kifo chake, Mogae alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya afya. Serikali ya Botswana ilitoa taarifa mwezi uliopita ikieleza kuwa alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali moja jijini Gaborone, ingawa haikuweka wazi ugonjwa uliokuwa ukimsumbua.
Enzi za utawala wake zilihusishwa na usimamizi mzuri wa uchumi, uwajibikaji serikalini pamoja na juhudi za kupambana na changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi nchini Botswana.
Kifo chake kimeacha simanzi kubwa nchini Botswana huku viongozi mbalimbali wakitarajiwa kutoa salamu za rambirambi kumuenzi kiongozi huyo wa zamani aliyekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa hilo.

.jpeg)



Post a Comment
"Karibu kutoa maoni yako. Kumbuka: Link zote za matangazo haziruhusiwi na zitafutwa kiotomatiki".