Serikali Kuandaa Sheria na Sera za Upandikizaji Viungo Nchini

Serikali imesema ipo katika hatua za mwisho za kuandaa mfumo wa kisheria pamoja na sera maalumu zitakazorasimisha huduma za upandikizaji wa viungo nchini Tanzania. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma hizo zinatolewa kwa viwango vinavyokubalika kisheria huku zikizingatia usalama na ubora wa huduma kwa wagonjwa.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Serikali, Grace Magembe, mchakato huo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Septemba mwaka huu. Amesema mfumo huo mpya utasaidia kuratibu huduma za upandikizaji viungo kwa ufanisi zaidi na kuweka misingi imara ya utoaji wa huduma hizo nchini.

Dk. Magembe ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa kongamano la kimataifa la kisayansi lililoandaliwa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa kwa lengo la kujadili sera, mikakati na mwelekeo wa kuboresha huduma za upandikizaji viungo Tanzania.

Amesema serikali inaendelea kutambua umuhimu mkubwa wa huduma za upandikizaji viungo hasa katika kipindi hiki ambapo mahitaji ya huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi yanaongezeka kwa kasi nchini.

“Serikali iko katika hatua za mwisho kuandaa sera na sheria zitakazoratibu huduma za upandikizaji viungo ili ziweze kutambulika rasmi na kutolewa kwa ufanisi zaidi,” amesema Dk. Magembe.

Aidha, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika sekta ya afya, hususan kwenye utoaji wa huduma za kibingwa, jambo ambalo limewawezesha wagonjwa wengi kupata matibabu ya hali ya juu ndani ya nchi bila kusafiri kwenda nje kutafuta huduma hizo.

Katika hatua nyingine, Dk. Magembe amewahimiza wananchi kujiunga na mifumo ya bima ya afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu. Amesema baadhi ya vifurushi vya bima tayari vimeanza kujumuisha huduma za upandikizaji viungo, jambo litakalosaidia kupunguza gharama kubwa za matibabu kwa wananchi wengi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa amesema kongamano hilo limewakutanisha wataalamu mbalimbali wa afya kujadili njia bora za kuendeleza huduma za upandikizaji viungo nchini. Pia limekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu pamoja na kujenga uwezo wa kitaalamu kwa wataalamu wa afya.

Ameongeza kuwa kongamano hilo linatarajiwa kuwa mwanzo wa maboresho makubwa ya kisera na kitaalamu yatakayosaidia kuongeza upatikanaji wa huduma bora za upandikizaji viungo kwa wananchi wa Tanzania.

WEKA COMMENT HAPA(Reply)

"Karibu kutoa maoni yako. Kumbuka: Link zote za matangazo haziruhusiwi na zitafutwa kiotomatiki".