Zaidi ya wananchi 1,300 wamegundulika kuwa na sonona
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema zaidi ya wananchi 1,300 wamegundulika kuwa na sonona na wanaendelea kupata matibabu, katika hatua inayoonyesha ukubwa wa changamoto ya afya ya akili nchini pamoja na juhudi zinazoendelea za Serikali kuimarisha huduma hizo kwa jamii.
Akizungumza Mei 11, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Mchengerwa alisema kuwa kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026 wananchi 1,709 walifanyiwa uchunguzi wa afya ya akili, ambapo watu 1,362 walibainika kuwa na sonona na tayari wanaendelea na matibabu.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali imeendelea kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu na huduma za afya ya akili kupitia wataalam wa afya ngazi ya jamii ili kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa waliopo katika maeneo ya vijijini na pembezoni.
Mchengerwa alisema mafunzo maalum yalitolewa kwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii 50 pamoja na wahudumu wengine wa afya 10 kwa lengo la kuwawezesha kutambua mapema changamoto za msongo wa mawazo na sonona, pamoja na kutoa msaada wa awali kwa wananchi wanaohitaji huduma hizo.
Alieleza kuwa hatua hiyo imelenga kusaidia kupunguza athari za matatizo ya afya ya akili ambayo yamekuwa yakiongezeka duniani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo changamoto za kiuchumi, msongo wa maisha pamoja na mazingira ya kijamii.
Mbali na sonona, Waziri huyo alisema Serikali pia imeendelea kutoa elimu kuhusu ugonjwa wa kifafa kupitia maadhimisho ya Siku ya Kifafa Duniani pamoja na mikutano mbalimbali ya kitaalamu, ambapo jumla ya watu 150 walifikiwa na elimu hiyo.
Aidha, wataalam 22 wa afya walipewa mafunzo kuhusu tiba na usimamizi wa wagonjwa wa kifafa ili kuongeza uwezo wa utoaji huduma bora kwa wagonjwa wanaokabiliwa na changamoto hiyo.
Katika hatua nyingine, Serikali imeendelea kutumia vyombo mbalimbali vya habari kutoa elimu kwa umma kuhusu afya ya akili, kifafa pamoja na changamoto nyingine zinazohusiana na afya ya akili kwa ujumla.
Mchengerwa pia alisema elimu kuhusu usonji ilitolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usonji Duniani, ambapo watu 247 walifikiwa na kupata uelewa kuhusu hali hiyo na umuhimu wa kuwasaidia watoto na watu wenye usonji katika jamii.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo wataalam wa afya wanaendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kutafuta msaada wa kitaalamu mapema wanapopata changamoto za afya ya akili badala ya kuficha matatizo hayo kutokana na hofu au unyanyapaa kutoka kwa jamii.





Post a Comment
"Karibu kutoa maoni yako. Kumbuka: Link zote za matangazo haziruhusiwi na zitafutwa kiotomatiki".