Cristiano Ronaldo kucheza na mwanawe Cristiano Ronaldo Jr katika timu ya Al Nassr msimu
Nyota wa soka duniani Cristiano Ronaldo (40) anaweza kuandika historia nyingine kubwa ya michezo iwapo atafanikiwa kucheza pamoja na mwanawe Cristiano Ronaldo Jr katika timu ya Al Nassr msimu ujao.
Ripoti kutoka vyombo vya habari vya Kiarabu zinasema kuwa klabu hiyo ya Saudi Arabia inaangalia uwezekano wa kumuinua kijana huyo mwenye umri wa miaka 15 kutoka timu za vijana na kumjumuisha kwenye kikosi cha wakubwa kutokana na maendeleo yake makubwa.
Cristiano Ronaldo Jr, ambaye tayari amewahi kucheza kwenye akademi za Real Madrid, Juventus na Manchester United, kwa sasa yupo kwenye mfumo wa vijana wa Al Nassr na ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao kwa wingi.
Cristiano Ronaldo Jr
Inadaiwa kuwa amefunga zaidi ya mabao 50 katika misimu tofauti akiwa kwenye timu za vijana, jambo lililovutia macho ya makocha na viongozi wa klabu hiyo.
Iwapo mpango huo utakamilika, Cristiano Ronaldo angeweza kuungana na mwanawe uwanjani hali ambayo ingekuwa nadra sana katika historia ya soka la kiwango cha juu duniani.
Tukio hilo lingemfanya Ronaldo kuiga mfano wa wanamichezo wachache duniani waliowahi kucheza pamoja na watoto wao katika ngazi ya juu ya ushindani.
Kwa sasa, Al Nassr inaendelea kufanya vizuri katika ligi ya Saudi Arabia na inaongoza msimamo, huku Ronaldo akiwa bado miongoni mwa wafungaji bora wa timu hiyo akiwa na mabao kadhaa msimu huu.
Hata hivyo, uamuzi wa mwisho kuhusu kupandishwa kwa Cristiano Ronaldo Jr utategemea tathmini ya maendeleo yake mwishoni mwa msimu.




