Showing posts with label Kimbunga Hidaya. Show all posts
Showing posts with label Kimbunga Hidaya. Show all posts

Mwenendo wa kimbunga HIDAYA kwa SasaAfyaclass Forum •

KIMBUNGA HIDAYA KINASOGEA HUKU KIKIPUNGUA NGUVU – TMA

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” kilichopo karibu na maeneo ya Pwani ya nchi ambapo hadi kufikia saa 9 usiku wa kuamkia leo, Kimbunga “HIDAYA” kilikuwa katika eneo la bahari takribani kilomita 125 kutoka Pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi), kilomita 93 kutoka pwani ya Mafia na kilomita 128 kutoka pwani ya Dar es Salaam kikiwa na mgandamizo wa hewa wa kiasi cha 985 hPa na kasi ya upepo unaofika kilomita 120 kwa saa.

Taarifa ya TMA imeeleza kuwa tangu usiku wa kuamkia leo, matukio ya upepo mkali na mvua kubwa zinazosababishwa na uwepo wa kimbunga “HIDAYA” yameendelea kujitokeza ambapo hadi kufika saa 3 asubuhi, kituo cha hali ya hewa cha Kilwa Masoko (Lindi) kimeripoti mvua ya jumla ya kiasi cha milimita 111.3 kwa kipindi cha masaa 6 yaliyopita.

Hata hivyo Kiwango hicho cha mvua ni kikubwa sana ukizingatia kuwa wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko ni milimita 96.6 tu.

TMA imesema kiasi cha mvua kilichonyesha ndani ya saa 24 katika kituo cha Kilwa Masoko ni takribani asilimia 115 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko.

Viwango vya mvua vilivyopimwa katika vituo vingine katika kipindi hicho ni milimita 90.7 kwa Mtwara na milimita 85.3 katika kituo cha hali ya hewa Naliendele (Mtwara).

Kiwango cha mvua cha milimita 90.7 kilichonyesha Mtwara ndani ya saa 24 ni takribani asilimia 168 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa Mtwara (milimita 54), vipindi vya mvua kubwa bado vinaendelea katika maeneo hayo ya ukanda wa Pwani ya Kusini.

Hata hivyo TMA imebainisha kuwa katika vituo vya hali ya hewa vya Mtwara, Kilwa, Zanzibar, Tanga na Dar es Salaam, upepo mkali unaozidi kilomita 50 kwa saa umeweza kupimwa katika nyakati tofauti kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi asubuhi hii.

Aidha, kimbunga “HIDAYA” kinatarajiwa kuendelea kusogea karibu zaidi na ukanda wa pwani ya nchi yetu huku kikipungua nguvu taratibu kuelekea usiku wa kuamkia Jumapili tarehe 05 Mei 2024.

Via:ITV

Mwenendo wa kimbunga HIDAYA kwa Sasa
0 Comment

Kimbunga Hidaya na kinachoendelea kwa sasaAfyaclass Forum •

Kimbunga Hidaya na kinachoendelea kwa sasa

Pwani ya Afrika Mashariki hususan Tanzania inatazamiwa kukumbwa na Kimbunga Hidaya ambacho kitasababisha mvua kubwa.

Mapema wiki hii Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitangaza kuwepo kwa mgandamizo mdogo wa hewa ambao ulitarajiwa kutawala na kusababisha mvua kubwa na upepo mkali katika mikoa mitano nchini ikiwa ni pamoja na Mtwara, Dar es Salaam, Lindi, maeneo ya Tanga, Morogoro, visiwa vya Pemba na Unguja pamoja na maeneo jirani.

Kimbunga Hidaya kilianza kujitengeza siku ya Jumatano kusini mwa Bahari ya Hindi kuelekea mashariki mwa Tanzania na kaskazini-mashariki mwa visiwa vya Komoro.

Kwa mujibu wa TMA, kufikia sasa mienendo ya mifumo ya hali ya hewa baharini bado inaonesha uwezekano mkubwa wa Kimbunga Hidaya kuendelea kusogea karibu na pwani ya Tanzania na kuendelea kuwepo hadi Jumatatu, Mei 6 2024.

Kulingana na mamlaka hiyo, kimbunga hicho kinaendelea kuimarika na kwamba hadi kufikia usiku wa kuamkia leo kasi yake ilikuwa imeimarika na kufikia kilomita 110 kwa saa.

Taarifa ya mamlaka hiyo aidha ilisema kwamba kimbunga hicho kitaendelea kuimarika na kuwa kikubwa zaidi katika saa 24 zijazo.

Tahadhari zilizotolewa na TMA?

Serikali imewashauri wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa ili kupata ushauri na mwongozo wa wataalamu katika sekta husika kwa lengo la kujikinga na athari zinazoweza kuibuka.

TMA imesema kwamba ongezeko la mvua na upepo mkali utakaoambatana na mawimbi makubwa baharini vinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani kuelekea tarehe 4 hadi 6 mwezi Mei 2024.

Kutokana na hilo, TMA imetoa tahadhari kwa wananchi katika maeneo husika na wote wanaojihusisha na shuguli mbalimbali baharini .

Vilevile Mamlaka hiyo imewataka Watanzania kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya Hewa.

Kenya imesema nini?

Serikali ya Kenya siku ya Alhamisi tarehe 2, Mei ilionya kwamba eneo la Pwani huenda likakumbwa na kimbunga Hidaya ndani ya siku chache zijazo kutokana na mvua kubwa inayoshuhudiwa kwa sasa kote nchini humo.

Onyo hilo lilitolewa baada ya kikao maalum cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Alhamisi kujadili hatua za ziada za kukabiliana na athari mbaya zinazoendelea za mafuriko, maporomoko ya udongo na maporomoko ya ardhi.

Baraza la Mawaziri lilifahamishwa kuhusu utabiri wa hali ya hewa kwa muda wa miezi mitatu ijayo, ambao ulionyesha kuwa mvua za wastani hadi juu ya wastani zitaendelea kunyesha katika maeneo yote ya nchi.

Kimbunga ni nini?

Kulingana na Shirika la Hali ya Hewa Ulimwenguni, kimbunga cha kitropiki – ni dhoruba inayozunguka kwa kasi ambayo huanza juu ya bahari ya kitropiki.

Kimbunga cha Kitropiki katika Bahari ya Hindi kina nguvu zaidi kuliko dhoruba ya kitropiki.

Ilipewa jina la ‘Hidaya’ na Meteo France La Reunion, huku mifano ya utabiri ikiifuatilia magharibi-kaskazini-magharibi kati ya Mei 2-4, 2024.

Kimbunga cha mwisho kuikumba Tanzania ilikuwa mwaka 1952 (wakati huo koloni la Tanganyika) na kilitua mkoani Lindi katika pwani ya kusini ya Tanzania.

Kimbunga cha mwisho kuikumba Zanzibar kilikuwa mwaka 1872 na athari zake zilifika mpaka upande wab ara katika eneo la Bagamoyo, kaskazini mwa Dar Es Salaam.

Ikiwa Kimbunga Hidaya kitatua kwa kasi, itakuwa ni mara ya kwanza katika historia kwa Dar Es Salaam kukumbwa na kimbunga.

Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania pia ilikuwa katika ya kupigwa na vimbunga vingine viwili, mwaka 2019 Kimbunga Kenneth kilitabiriwa kupiga mkoa wa Mtwara lakini hata hivyo kilibadili mwelekeo na kutua nchini Msumbiji.

Mwaka 2021 ilitolewa tahadhari ya Kimbunga Jobo lakini hata hivyo kilipunguza makali na hakikusababisha maafa yeyote makubwa.

Kimbunga Hidaya na kinachoendelea kwa sasa
0 Comment

Kenya Mafuriko, shughuli za baharini zazuiwa tahadhari ya Kimbunga HidayaAfyaclass Forum •

Kenya Mafuriko, shughuli za baharini zazuiwa tahadhari ya Kimbunga Hidaya

Wakazi wa kaunti ya Lamu hawataruhusiwa kusafiri baharini kuanzia leo jioni hadi siku ya Jumanne kufuatia tahadhari ya Kimbinga Hidaya.

Wavuvi na abiria wameshauriwa kukatiza safari zao.

Viongozi wa Lamu walikutana kujadili namna ya kuepuka maafa wakati Kimbunga Hidaya kikitarajiwa.

William Samoe, Kamanda wa Polisi eneo la Lamu ametoa wito kwa wakaazi kutii maagizo wanayopewa na kwamba suala hili litachukuliwa kwa uzito mkubwa.

Abiria kwa sasa wametakiwa kuvaa majaketi ya kuokoa maisha na pia kutopakia abiria wengi kupita kiasi kwasababu kwasasa bahari itakuwa inashuhudia mawimbi makali na mvua.

Chanzo: Bbc

Kenya Mafuriko, shughuli za baharini zazuiwa tahadhari ya Kimbunga
Hidaya
0 Comment
Notification
My blog is in the process of editing and perfecting the new template, so there are still some functions to click but not yet used. Note which blogs associated with your side please read this lesson to update the blog logo.
UNDERSTOOD