Showing posts with label Ugonjwa wa macho mekundu. Show all posts
Showing posts with label Ugonjwa wa macho mekundu. Show all posts

Mlipuko wa ugonjwa wa macho,Macho MekunduAfyaclass Forum •

Mlipuko wa ugonjwa wa macho,Macho Mekundu

Baada ya Ugonjwa huu wa macho kusumbua watu wengi kwa kipindi cha Hivi Karibuni, ndani ya Afyaclass tulitoa elimu mbali mbali kuhusu Ugonjwa huu,

Na leo Katika Makala hii tunazidi kukuelimisha Uujue Vizuri Ugonjwa huu wa macho Mekundu Maarufu kama RED EYES.

Ugonjwa wa Macho Mekundu(RED EYES),chanzo,dalili na Matibabu

Ugonjwa wa macho mekundu ni ugonjwa ambao hujulikana kama Red Eyes,

Ugonjwa wa red eyes ni ugonjwa ambao huhusisha macho kuwa mekundu kama dalili kubwa.

Katika Makala hii tumechambua chanzo cha Ugonjwa wa macho mekundu(Red Eyes), dalili Zake kuu, jinsi ya kuzuia usipate Pamoja na Matibabu yake.

CHANZO CHA UGONJWA WA MACHO MEKUNDU

Ugonjwa wa Macho mekundu(Red Eyes) hutokana na mashambulizi ya vimelea vya magonjwa kama vile Virusi ambavyo husababisha vishipa vidogo ndani ya macho kuvimba na kupasuka, kisha damu kuvilia ndani ya jicho.

Maambukizi ya kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho yajulikanayo kitaalam “Viral Keratoconjunctivitis” ni Maambukizi yanayosambaa kwa kasi kubwa .Hakuna tiba maalum kwa ugonjwa huu na hata bila tiba, dalili huisha zenyewe ndani ya wiki mbili . Usafi ni jambo muhimu katika kuzuia maambukizi haya kusambaa kwa wengine.

Mlipuko huu husababishwa na Kirusi kijulikanacho kwa jina la “Adenovirus”kwa zaidi ya asilimia 80%.

Dalili za Ugonjwa wa Macho Mekundu

DALILI ZA UGONJWA WA MACHO MEKUNDU NI PAMOJA NA;

• Macho kubadilika rangi na kuwa mekundu,

hii ni ishara ya Vishipa vidogo vya damu ndani ya macho kuvimba na kupasuka, kisha damu kuvilia ndani ya jicho.

• Kuwashwa na macho

• Kuhisi kitu kama mchanga ndani ya jicho lako

• Kuvimba macho yako

• Kuhisi hali ya kuungua ndani ya macho,

Hii ni ishara ya kutengeneza hali ya vidonda ndani ya jicho(Conjunctivitis Sore),

• Macho kuwasha au kutoa maji/nachozi yenyewe n.k

Ni nini cha Kufanya Kama Una Ugonjwa wa Macho Mekundu(Red Eyes)?

Ikiwa jicho lako haliumi na kuona kwako hakujaathiriwa, labda sio jambo kubwa. Ugonjwa huu wa macho mekundu(Red Eyes) unaweza kupona wenyewe ndani ya siku chache.

Mpaka Unapona Unashauriwa;

  • Kutokugusa au kusugua macho yako
  • Usivae miwani inayogusa macho, na kama kuna ulazima wa kuvaa,Hakikisha miwani yako(contact Lenses) inakuwa Safi, na Usiivae kwa muda mrefu Zaidi ya inavyoshauriwa
  • Zingatia Usafi

JINSI YA KUZUIA UGONJWA WA MACHO MEKUNDU

– Watoto wadogo Wagonjwa wanaoenda shule wanashauriwa wakae nyumbani hadi dalili zinapoisha kwa kuwa ni ngumu kuzuia maambukizi yasisambae kwenye mazingira ya shule.

– Watu wazima wanaweza kwenda kazini ila wanapaswa kuzingatia kanuni za kuzuia kutokuambukizwa au kuambukiza wengine kwa kufuata kanuni za kuzuia maambukizi.

– Watumishi wa Afya wazingatie kutopeleka Maambukizi hayo nyumbani kwa kufuata kanuni za kuzuia maambukizi.

Zingatia Zaidi Mambo Haya Muhimu;

1. Usisugue au kupikicha macho yako,

Uchafu pamoja na Viini vya magonjwa(germs) kwenye mikono yako pamoja na Vidole vinaweza kusababisha hali Zaidi ya Wekundu na Muwasho ndani ya macho.

2. Kama unavaa miwani, Hakikisha miwani yako(contact Lenses) inakuwa Safi, na Usiivae kwa muda mrefu Zaidi ya inavyoshauriwa

3. Zingatia Usafi kwa Ujumla, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mikono yako unanawa kwa maji safi tiririka na Sabuni

4. Kwa Wale wanaopaka MakeUp, Hakikisha unaondoa MakeUp yako Vizuri na kuacha macho yako yakiwa Safi(Remove your eye makeup properly, and keep your eyes clean).

5. Pata Mapumziko ya mara kwa mara, ikiwa unafanya kazi zinazohusisha kuangalia computer screen kwa Muda Mrefu.

6. Epuka vitu ambavyo huweza kuleta usumbufu(irritation) wowote machoni kama vile; vumbi,moshi n.k

7. Hakikisha unaenda kuchunguzwa macho au kufanya Vipimo vya macho(Eye exam) ikiwa una shida ya macho kuwa mekundu mara kwa mara au Ikiwa hali ya macho kuwa mekundu haiishi.

MATIBABU YA UGONJWA WA MACHO MEKUNDU(RED EYES)

– Ugonjwa huu wa Macho mekundu(red eyes) hupona wenyewe ndani ya siku 3 mpaka 5, ndani ya wiki 2 n.k kulingana na uwezo au uimara wa kinga yako ya mwili Wala huhitaji matumizi ya dawa yoyote ile.

Japo lazima kwanza kuchuguzwa na wataalam wa afya baada ya kujihakikishia kuwa ni shida ya red eyes watakupa maelekezo kwa kina ikiwa ni pamoja na jinsi ya kutunza jicho lako.

KWA USHAURI ZAIDI,ELIMU AU TIBA JUU YA TATIZO LOLOTE LILE TUWASILIANE KWA NAMBA +255758286584.

Mlipuko wa ugonjwa wa macho,Macho Mekundu
0 Comment

Red Eyes yapofusha Saba Dar wakati wakiitibuAfyaclass Forum •

Red Eyes yapofusha Saba Dar wakati wakiitibu

 Idadi inafanya jumla ya wagonjwa waliougua macho mekundu na kupata  madhara  kwa Tanzania Bara na Zanzibar kufikia 14.

Wizara ya Afya imesema watu saba jijini Dar es Salaam wamepata upofu kutokana na kutibu ugonjwa wa macho mekundu kwa njia za kienyeji, huku wawili kati yao vioo vya jicho vikitoboka.

Ugonjwa huo wa maambukizi kwenye ngozi ya juu ya gololi la jicho unaoitwa Conjunctivitis, maarufu Red eyes umesambaa mikoa 26 nchini.

Februari 7, 2024, mratibu wa huduma za afya msingi na matibabu ya macho Zanzibar, Dk Rajab Muhammed Hilali alitoa takwimu za watu saba kupata upofu baada ya matumizi ya dawa za kienyeji kutibu ugonjwa huo.

Athari za kutibu ugonjwa wa macho kwa njia asili

Idadi hiyo inafanya jumla ya wagonjwa waliopata madhara hasi kwa Tanzania Bara na Zanzibar kufikia 14.

Ugonjwa huo ulioripotiwa kwa mara ya kwanza Januari 13, 2024 athari zake hasi ni vidonda kwenye kioo cha jicho vinavyoweza kusababisha kovu kwenye jicho litakalomfanya mgonjwa apate uoni hafifu au kupoteze uwezo wa kuona kabisa.

Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Jumapili Februari 18, 2024, Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya, Profesa Paschal Ruggajo amesema hadi Februari 15, watu saba walitolewa taarifa ya kupata madhara kwenye vioo vya jicho.

“Watano wamepata vidonda kwenye kioo cha jicho na wawili walikutwa vioo vya jicho vimetoboka. Wagonjwa wote walionwa kwenye vituo vya tiba vilivyopo Dar es Salaam na umri wao ni kati ya miaka 21 hadi 42.

“Baadhi ya vitu vilivyotumika na waathirika hao ni pamoja na maji ya chumvi, tangawizi, maji ya majani ya mbaazi, vitunguu swaumu, chai ya rangi, vicks na dawa zenye viambata vya steroids,” amesema Ruggajo.

Profesa Ruggajo amesema wizara imeendelea kufuatilia mwenendo wa maambukizi na kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna bora ya kujikinga na ugonjwa huo.

Amesema hadi Februari 15 2024, jumla ya wagonjwa 14,641 wametolewa taarifa, walioonwa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwenye mikoa 26.

Dar es Salaam inaongoza kwa idadi ya wagonjwa 6,940, Pwani (4,480), Morogoro (630) na Dodoma (550).

Profesa Ruggajo amesema wizara inaendelea na hatua mbalimbali za kinga na udhibiti wa ugonjwa huo, ikiwamo utoaji wa elimu kwa kutumia wataalamu wa afya kupitia vyombo vya habari.

“Elimu inatolewa maeneo yenye mikusanyiko hususani shule, magereza na vyuo, nyumba za ibada, usambazaji wa vipeperushi na utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa kupitia vituo vyetu vya tiba na mitandao ya kijamii,” amesema.

Amesema wizara pia inaendelea kuratibu na kusimamia huduma mkoba za macho kwenye maeneo mbalimbali nchini na kubaini wagonjwa wenye shida ya macho mekundu na kuwapatia elimu.

“Hadi sasa vipindi vya kwenye runinga zaidi ya 20 vimetolewa na wataalamu wetu wa afya, redio za kijamii zaidi ya 25 kwenye mikoa mbalimbali, ikiwemo ambayo haina wagonjwa,” amesema.

Amesema wanafunzi wa shule za msingi na sekondari zaidi ya 25,000 wamefikiwa kwenye shule zao pamoja na walimu wao.

Profesa Ruggajo amesema wanaendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya kutofuata kanuni zilizotolewa, baada ya kupata taarifa ya wagonjwa kutumia tiba zisizo rasmi na kupata madhara.

Kutokana na hilo, amesema wizara iliandaa video na kuirusha kwenye vyombo mbalimbali vya kuelimisha.

Akizungumza na Mwananchi Februari 8, 2024, Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho, Wizara ya Afya, Dk Bernadetha Shilio alisema baadhi ya wagonjwa wanaopokewa kioo cha jicho kinabainika kumeharibika.

Amesema wagonjwa wa aina hiyo wanapotibiwa bado kunakuwa na kovu lenye rangi nyeupe kama karatasi ambalo likibaki hivyo moja kwa moja hupata ulemavu wa kutoona.

Matibabu sahihi:

Wizara inaelekeza hatua za kuchukua kwa kuosha uso kwa maji safi na sabuni mara kwa mara.

Tumia dawa ya paracetamol kumeza kwa ajili ya kupunguza maumivu

Nenda kituo cha tiba kwa ajili ya uchunguzi, kama hupati nafuu.

Hakikisha mikono na uso inakuwa safi muda wote.

Jizuie kugusa macho yako kadri uwezavyo.

Tumia vipukusi (vitakasa mikono) mara kwa mara.

Epuka kushikana mikono au kugusa vitu vinavyoguswa na wengi.

 Tumia taulo au leso za karatasi kufuta tongotongo au machozi.

Nenda kituo cha kutolea huduma mara upatapo dalili.

Kumbuka kufua mashuka na mataulo kila siku.

Via:Mwananchi

Soma Zaidi kuhusu Red eyes;

Red Eyes yapofusha Saba Dar wakati wakiitibu
0 Comment

Dawa zisizo rasmi za macho mekundu(Red Eyes) zitawapa UpofuAfyaclass Forum •

Dawa zisizo rasmi  za macho mekundu(Red Eyes) zitawapa Upofu

Serikali kupitia Wizara ya Afya imewaasa Wananchi kuacha tabia ya kutumia dawa zisizo rasmi za macho kwa lengo la kutibu ugonjwa wa macho mekundu (Red Eyes),

kwakuwa matumizi hayo yanaweza kupelekea upofu usiotibika kama ambavyo itakuwa kwa wengi wa Wagonjwa waliokwisha kupata madhara kwenye kioo cha jicho kwa kutumia vitu hivyo.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya Prof. Paschal Ruggajo amesema hayo leo Jijini Dar es salaam ambapo amesema ugonjwa wa ‘Red Eyes’ hauleti upofu lakini matumizi ya dawa zisizo rasmi na zinazonunuliwa kiholela yanaweza kupelekea upofu usiotibika kama ambavyo inaweza kuwapata baadhi ya Wagonjwa waliopata vidonda kwenye kioo cha jicho baada ya kutumia dawa hizo zisizo rasmi.

Amesema baadhi ya vitu vinavyotumika ni pamoja na dawa zenye vichocheo vya ‘steroids’ ambazo Wananchi wanakwenda kununua wenyewe kwenye maduka ya dawa, tangawizi, chai ya rangi illiyokolea majani, mafuta tete yaliyokuwa yakitumika wakati wa janga la Covid – 19, maji ya chumvi na maziwa ya Mama, ambavyo vitu vyote hivyo sio salama na havijaelekezwa na Wataalamu.

Wizara imeendeleza kusisitiza Jamii kuzuia kuenea kwa maambukizi haya kwa kuzingatia usafi binafsi na kanuni za afya ikiwa ni pamoja na usafi wa mikono na uso, kuzuia kugusa macho , kunawa mikono na maji tiririka na sabuni au kutumia vipukusi mara kwa mara, kuzingatia kutokushikana mikono maeneo ya sehemu za ibada, kutumia taulo au leso za karatasi kufuta tongotongo au machozi na kufika kwenye kituo cha kutolea huduma pale Mtu apatapo dalili za Red Eyes.

Soma Zaidi; Ugonjwa wa macho mekundu(Red eyes)

Dawa zisizo rasmi za macho mekundu(Red Eyes) zitawapa Upofu
0 Comment

Fahamu hapa,Masharti mapya ya kukabiliana na kipindupindu pamoja na ‘red eyes’Afyaclass Forum •

Fahamu hapa,Masharti mapya ya kukabiliana na kipindupindu pamoja na ‘red eyes’

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu amezitaka nyumba za ibada kusitisha utaratibu wa waumini wake kushikana mikono, ikiwa ni sehemu ya kupambana na magonjwa ya mlipuko ya viral keratoconjunctivitis (red eyes) na kipindupindu.

Profesa Nagu alisema hayo jana, wakati akiongoza kikao cha 10 cha Bodi ya Ushauri wa Hospitali Binafsi.

Pia, alitoa rai ya matumizi ya majisafi tiririka na sabuni maeneo ya mikusanyiko, ofisi za umma na binafsi, nyumbani na sehemu za biashara, huku akiwahimiza wanaotumia vyombo vya usafiri kutumia vitakasa mikono.

Profesa Nagu alisema hayo baada ya kuwapo ongezeko la wagonjwa wa macho unaoambukizwa kwa kushikana mikono, kugusa sehemu aliyogusa mwenye maambukizo ambalo kwa sasa imefikia mikoa 17 na ugonjwa wa kipindupindu umesambaa katika mikoa 14.

“Muhimu kuzingatia usafi wa mtu binafsi na mazingira, tuepuke kushikana mikono, hasa katika nyumba za ibada sitisheni huu utaratibu kwa muda,” alisema Profesa Nagu.

“Maeneo ya mikusanyiko tusishikane mikono, wekeni miundombinu ya kunawa maji tiririka na sabuni, agizo hili ni kwa watu wote wa majumbani, sehemu za biashara, kwenye mikusanyiko, ofisi za umma na binafsi.”

Januari 29, Wizara ya Afya ilisema jumla ya mikoa 17 imeathirika na ugonjwa wa macho mekundu.

Akitoa taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo alisema hadi kufikia Januari 26 mwaka huu, idadi ya waliofika kwenye vituo vya afya walikuwa 5,359 kutoka 1,109, Januari 19.

“Ugonjwa huu umesambaa zaidi, ingawa ni wachache ndio wanafika vituo vya huduma za afya, mpaka sasa ugonjwa huu umesambaa na kuongezeka katika mikoa 17, ikiwamo ya Singida, Katavi, Kilimanjaro, Mara, Iringa, Njombe, Ruvuma, Simiyu, Mtwara, Lindi, Songwe, Rukwa na Mwanza,” alisema Profesa Rugajjo.

Akizungumza jana, Profesa Nagu alisema Serikali imechukua hatua nyingi, ikiwamo kuhakikisha kuna upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote yaliyoathirika na kushughulikia miundombinu ya majitaka ili kuhakikisha inakuwa vizuri.

“Kwa sababu ya mvua, miundombinu mingine ya maji taka inafunikwa, hivyo jitihada kubwa zimefanyika kuhakikisha inafukuliwa na timu ya wataalamu wa elimu ya afya kwa jamii wapo maeneo yote wakihimiza usafi wa mtu binafsi na mazingira,” alisema Profesa Nagu.

Alisisitiza watumiaji wa usafiri wa vyombo vya moto vya kuchangia, kutembea na vitakasa mikono, huku akihamasisha unywaji wa majisafi na salama pamoja na kuosha matunda na mbogamboga kuepuka maambukizi.

Profesa Nagu alisema mlipuko wa magonjwa hayo umetokana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa kuna mvua zilizozidi kiwango, miundombinu imebadilika na kutokea kwa milipuko ya magonjwa duniani kote.

Alisema kipindupindu si Tanzania pekee, bali kimeathiri nchi kadhaa, ikiwamo Zambia ambayo mpaka sasa shule zimeshindwa kufunguliwa.

“Baadhi ya mikoa tumefanikiwa kudhibiti ugonjwa huu, lakini bado tunapambana katika mikoa michache ya Mwanza, Katavi na Kagera, hatua zinapaswa kuchukuliwa na wananchi wenyewe kwa kujikinga, mvua bado zinakuja,” alisema.

Imani potofu

Chanzo cha kusambaa kwa kipindupindu wilayani Sengerema Mkoa wa Mwanza hadi kufika watu 61, imeelezwa ni kutokana na kuwepo kwa imani potofu kwa jamii kuwa wakitumia dawa za kienyeji kujikinga zitasaidia kupona ugonjwa huo.

Sakata hilo liliibuka jana, kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Sengerema, kilichokuwa kikijadili na kupitisha rasimu ya bajeti ya mwaka 2024/25.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Binuru Shekidele alisema timu ya wataalamu wa afya ilikwenda maeneo yaliyoathirika kwa ajili ya kutoa huduma za afya na kujikinga na baadaye ilibaini wananchi wakitumia njia isiyo sahihi kujitibu na kujikinga.

“Kusambaa kwa ugonjwa huu, kumetokana na imani potofu kwa wananchi kutumia dawa za kienyeji za kuvaa kiunoni na kushindwa kufuata kanuni za afya, wakisema zitawasaidia,” aliseme Shikidele.

Tangu kuibuka kwa kipindupindu, Wilaya ya Sengerema wameripotiwa wagonjwa 61 kutoka Januari 30 hadi Februari 2, mwaka huu.

Kati yao, 27 wamepona na kuruhusiwa, huku 34 wakiendelea kulazwa kwa matibabu kwenye vituo vya afya wilayani humo.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga amepiga marufuku uuzwaji wa vyakula holela shuleni, sambamba na mikusanyiko kwenye misiba.

Ugonjwa huo kwa sasa unasambaa kwa kasi kwenye maeneo yaliyopo pembezoni mwa Ziwa Victoria, yakiwamo ya Chifunfu, Kijiji cha Kiweni, Kata ya Kasenyi, Kijiji cha Lugongo na Mbalagane na Kata ya Katunguru.

Kisababishi kingine kilichotajwa ni wakazi wa mwambao wa ziwa kujisaidia hovyo.

Mmoja wa wananchi wa Kata ya Kasenyi, Anastazia John alisema ni kweli jamii ya wananchi wa kandokando mwa Ziwa Victoria wanaamini dawa za kienyeji zinatibu kuzuia magonjwa mbalimbali kuliko dawa zinazopatikana kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

“Elimu inahitajika kwa jamii kuachana na imani potofu na kufuata kanuni za afya ili kuepuka kupata magonjwa ya mlipuko,” alisema Annastazia.

Baadhi ya madiwani waliwaomba wataalamu wa afya kuweka nguvu kwenye maeneo yaliyoathirika na ugonjwa huo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Thomas Rutachunzibwa yuko Sengerema na timu ya afya ya mkoa, wakishirikiana na ya wilaya hiyo katika kata zilizoathirika.

Alipoulizwa hali ya kipindupindu mkoani Mwanza, Mratibu Elimu ya Afya wa Mkoa huo, Renard Mlyakado bila kutaja takwimu za mkoa mzima, alisema ugonjwa huo bado upo, akiwataka wananchi waendelee kuchukua tahadhari.

Aliwaomba wananchi kuacha utaratibu wa kusalimiana kwa kushikana mikono ili kuepuka kula bakteria, akidai hawawezi kujua wanaoshikana nao kama wana bakteria mikononi au la.

“Muhimu ni usafi wa mazingira na vyoo bora. Hata kama mtu ana choo cha shimo basi ahakikishe anakifunika ili inzi asitoe bakteria kwenye kinyesi na kusambaza kwa wakazi husika,” alisema Mlyakado.

Fahamu hapa,Masharti mapya ya kukabiliana na kipindupindu pamoja na
‘red eyes’
0 Comment

Mkojo,Chumvi, kitunguu saumu sio dawa ya kutibu ‘red eyesAfyaclass Forum •

Mkojo,Chumvi, kitunguu saumu sio dawa ya kutibu ‘red eyes’

Wataalamu wasema zinachangia kuongeza maumivu, waonya zaweza kusababisha uoni hafifu na upofu.

Wataalamu wa afya na madaktari bingwa wa macho wamesema wanapokea idadi kubwa ya wagonjwa wakiwa katika hali ya ugonjwa mkali, kutokana na matumizi ya njia mbadala kutibu macho, ikiwamo matumizi ya mkojo na chumvi.

Hali hiyo imebainika siku 15 tangu kutangazwa kuibuka ugonjwa huo ujulikanao viral keratoconjunctivitis (red eyes) Januari 13, 2024 mkoani Dar es Salaam.

Wataalamu waliozungumza na Mwananchi Digital jana Januari 28, 2024 wameeleza wagonjwa wanaotumia chumvi, mkojo, chai ya rangi na kitunguu saumu kama tiba, macho yao huvimba na kuuma zaidi pamoja na kupatwa homa. Athari hasi zaidi zinazotajwa ni kusababisha vidonda kwenye kioo cha jicho.

Tiba hizo mbadala zinaelezwa zinaweza kusababisha kovu kwenye jicho litakalomfanya mgonjwa apate uoni hafifu au kupoteze uwezo wa kuona kabisa.

Daktari bingwa na mkuu wa kitengo cha macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Sarah Mrema ameisema idadi ya wagonjwa wanaohudhuria hospitalini hapo kutibiwa macho imekuwa ikiongezeka na kupungua.

Amesema wamekuwa wakipokea wagonjwa wakiwa tayari walianza kutumia tiba za majani ya chai, vitunguu saumu na chai ya rangi.

“Si kwamba wanapona wakitumia tiba mbadala, maumivu yanazidi, wakija hapa wanakuwa na maumivu makali. Ukihoji anakwambia alitumia mkojo, chumvi na njia nyingine nyingi. Unampa dawa anatumia, kisha anapona,” amesema Dk Sarah.

Kwa mujibu wa Dk Sarah, takwimu za hospitali hiyo zinaonyesha tangu Desemba 22, 2023 wagonjwa 105 walifika kutibiwa na kuna siku orodha ya wagonjwa inapanda na siku nyingine inapungua.

Daktari bingwa wa macho katika Hospitali ya Muhimbili-Upanga, Neema Moshi amesema unapotumia vitu vikali kutibu macho, ni rahisi kuharibu kioo cha mbele cha jicho na maumivu yanayotokea huwa makali.

Amesema wakati mwingine unaweza kupoteza uoni kwa sababu ya kuharibu kioo hicho.

“Tunapokea wagonjwa wengine wana hali mbaya, lakini hawezi kuwa mkweli, unajua mgonjwa hawezi kuja kusema alitumia kitu fulani, mara nyingi wanafichaficha labda tatizo liwe kubwa zaidi ndipo wanasema ukweli,” amesema.

Dk Neema amesema kama mgonjwa ametumia vitu hivyo na hajapata athari hawezi kupata athari baadaye.

“Si kwamba athari hizo zinakuwa za taratibu, kama amepona na haikuonekana kupata shida yoyote haiwezi kutokea tena baadaye,” amesema.

Meneja Mpango wa Taifa wa huduma za macho kutoka Wizara ya Afya, Dk Bernadetha Shilio amesema wapo wagonjwa wanaopata athari, lakini hawana takwimu, akisisitiza ni muhimu wagonjwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu.

“Taarifa hizi zinatolewa na wataalamu wa afya, yaani madaktari kwenye vituo husika, labda mimi kuna mtu amekuja amefanya hivi na vile lakini kutoa hali ilivyo kwa sasa wangapi wamethirika kwa sasa bado.

“Hata leo nimepewa taarifa kuna mtu anatumia sijui vitu gani, lakini pia kuna taarifa za uvumi kuna mtu katoka huko anashauri wagonjwa wanywe Azuma inatibu, huo ni uongo,” amesema.

Dk Shilio amewataka wagonjwa waepuke kutibu macho kwa kutumia kitunguu saumu kwa kuwa kunaweza kusababisha michubuko kwenye ngozi ya jicho na kioo cha mbele ya jicho, hivyo kuathiri uwezo wa jicho kuona.

“Maji ya chumvi yanaweza kusababisha michubuko au kidonda kwenye kioo cha mbele cha jicho, hivyo kutengeneza kovu litakalopunguza uwezo wa jicho kuona au ulemavu wa kutoona wa kudumu,” amesema.

“Matumizi ya chai ya rangi katika kutibu macho yanaweza kusababisha vidonda kwenye kioo cha jicho na kusababisha kovu kwenye jicho litakalokufanya upate uoni hafifu au upoteze uwezo wa kuona kabisa,” amesema.

Dk Shilio amewataka wagonjwa pia kuepuka kutibu macho kwa mkojo, kwani ni hatari kwa usalama wa macho kwa kuwa mkojo hubeba uchafu na vijidudu vinavyoweza kusababisha maambukizi mengine na kupoteza uwezo wa kuona kabisa.

Amewataka kuzingatia kunawa mikono mara kwa mara na wapatapo ugonjwa huo kuwahi kituo cha afya kwa uchunguzi na matibabu sahihi na kwa wakati.

Via Mwananchi.

Soma Zaidi hapa Dawa ya Kutibu Ugonjwa wa macho mekundu(Red Eyes)

Mkojo,Chumvi, kitunguu saumu sio dawa ya kutibu ‘red eyes
0 Comment
Notification
My blog is in the process of editing and perfecting the new template, so there are still some functions to click but not yet used. Note which blogs associated with your side please read this lesson to update the blog logo.
UNDERSTOOD