Chama cha Walimu Tanzania (CWT) chapata raisi mpya
Hatimaye tambo na majigambo ya wagombea nafasi ya urais, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) zimekwisha baada Suleiman Ikomba kutangazwa mshindi akimbwaga Leah Ulaya.
Wawili hao walikuwa wamevuta hisia za walimu, huku tambo za kila namna zikisikika mitaani na ndani ya Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma ambao kwa siku tatu ulikuwa na ulinzi kila kona.
Kwa uchaguzi huo ulioanza asubuhi ya jana Jumatatu, Juni 9, 2025 na matokeo kutangazwa alfajiri ya leo Jumanne, Juni 10, 2025, CWT itapaswa kuitisha uchaguzi mwingine katika kipindi cha miaka miwili ijayo kutokana na katiba yao, ili kuziba nafasi ya rais kwa kuwa, umri wa miaka 58 wa Ikomba hautamfikisha mwaka 2030.
Wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), wakifurahia baada ya Suleiman Ikomba kutangazwa rais mpya.
Katiba ya CWT inatambua mwanachama halali ni yule atakayechangia asilimia mbili ya mshahara wake katika chama hicho, lakini rais huyo mpya atastaafu utumishi baada ya miaka miwili, hivyo atapoteza sifa za kuwa kiongozi.
Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi huo, Halima Liveta amemtangaza Ikomba kuwa rais kwa kupata kura 608 dhidi ya 260 alizozipata aliyekuwa rais wa awamu iliyopita Leah, wakati kura moja ikiharibika.
The former President of the Tanzania Teachers’ Union (CWT), Leah Ulaya, addresses members after the union’s election concluded at the Jakaya Kikwete Convention Centre in Dodoma.
Jumla ya wapigakura walioripoti kwenye uchaguzi huo walikuwa 914 lakini waliopiga kura ni 868.
Kabla ya kukwaa nafasi hiyo, Ikomba alikuwa makamu wa rais wa CWT aliyechukua nafasi ya Dinna Mathamani aliyeingia kwenye mgogoro, lakini baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
"Komredi Leah Ulaya amepata kura 260 na komredi Suleman Ikombo amepata kura 608, kwa matokeo haya namtangaza mshindi Ikomba kuwa mshindi wa kiti cha rais wa chama chetu," amesema Liveta.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Ikomba ameomba wanachama wa CWT kumaliza makundi ya uchaguzi ili kukijenga chama imara kisichokuwa na mipasuko.
"Kwanza tumshukuru Mungu uchaguzi tumemaliza salama, hivyo niwaombe tumalize makundi ambayo tuliyatengemeza katika uchaguzi na tumemaliza salama kila kitu kiishie hapa tuanze kujenga CWT imara," amesema Ikomba.
Kwa upande wake, Leah amewashukuru wajumbe namna walivyompa ushirikiano tangu alipoanza kuongoza CWT huku kiwaomba viongozi kudumisha mshikamano na kumaliza makundi.
PiIi, ametaka watazame ni kwa nini walimu wengi wanazidi kuhama ndani ya CWT na kujiunga na chama kipya na tatu, ameomba viongozi kudumisha upendo.
Kwenye uchaguzi huo, Joseph Misalaba ameshinda nafasi ya katibu mkuu akiwaacha mbali wagombea wengine Jeston Benjamin, Abihudi Bukuku na Simon Keha.
Kabla ya hapo Misalaba alikuwa akikaimu nafasi hiyo kutoka kwa Maganga aliyekuwa akikaimu baada ya Katibu Mkuu Deus Seif kuingia mgogoro na kashfa ya matumizi mabaya ya ofisi.
REPLY HAPA
image quote pre code