CHAMA cha Mtindo Maalum wa Uzungumzaji Tanzania (CHAMMUTA) kitaanza kambi maalum ya watoto wenye kigugumizi itakayofanyika Dar es Salaam huku lengo ni kuwahudumia watoto na vijana kuzungumza kwa kujiamini.
Kambi hiyo itaanza Juni 23 hadi 27 mwaka huu na inatarajia kupokea watoto kati ya 30 na 50 wenye kigugumizi.
Akizungumza leo Dar es Salaam, mratibu wa kambi hiyo, Dudley Mbowe amesema watoto wenye kigugumizi wanahitaji mazoezi ya kuzungumza kwa kujiamini, ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wanasaikolojia na wataalamu wa mawasiliano na kuwajengea uwezo wa kuwa mabalozi wa kuielimisha jamii kuhusu kigugumizi.
Mbowe amesema kaulimbiu ya ‘’Ota, zungumza, ishi’’ inalenga kuwahamasisha watoto na vijana kutambua ndoto zao, kuzungumza kwa ujasiri na kuishi maisha kamili bila woga wala aibu.
‘’Tunaamini kuwa kila mtoto au mtu ana haki ya kusikilizwa, kueleweka, na kuheshimiwa bila kujali changamoto yake ya maisha ikiwemo kigugumizi,’’ ameeleza Mbowe.
Amesema ulemavu ni hali halisi inayowakumba watoto na watu wazima wengi na kuwafanya watoto kutohudhuria darasani na katika maisha mengine ya kila siku.
‘’Kambi hii itakuwa nafasi ya kipekee ya kuondoa unyanyapaa na kuwawezesha watoto kuota maisha bora si tu kwa kujieleza bali pia kuwa mabalozi wa kuelimisha wengine,’’ amesisitiza.
Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Chama hicho, Ally Baharoon ameyataka mashirika ya kijamii, sekta ya afya na elimu, sekta binafsi, wahisani, wazazi na walkezi wa watoto wenye kigugumizi kushiriki katika kambi hiyo.
Amesema kupitia kambi hiyo, wanatarajia kuleta mabadiliko chamnya kwa watoto, vijana na watu wote sambamba na kuwajengea hali ya kujiamini na kuwa sehemu ya jamii inayoelewa, kukubali na kusaidia maendeleo ya watu.
‘’Vyombo vya habari mna nafasi ya kuelimisha jamii, kusaidia kuvunja mitazamo potofu kuhusu kigugumizi na kuchangia kujenga jamii jumuishi,’’ amesisitiza Baharoon.
REPLY HAPA
image quote pre code