Mtanzania apenya Nafasi za Juu katika Utawala wa Kanisa Katoliki duniani
Uteuzi wa Monsinyo Mbena unamfanya kuwa mmoja wa Watanzania wachache waliowahi kushika nafasi za juu katika utawala wa Kanisa Katoliki duniani.
Papa Leo XIV amemteua Mtanzania, Mosinyo Romanus Mbena kuwa Mkuu wa Ofisi ya Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo, nafasi yenye hadhi kubwa katika Kanisa Katoliki duniani, yenye jukumu la kusimamia misaada na huduma za kichungaji kwa maskini na wahitaji.
Taarifa kutoka Vatican zinasema uteuzi huo unaanza rasmi Juni 1, 2025, huku Mbena akichukua nafasi hiyo baada ya miaka mingi ya kulitumikia Kanisa katika huduma ya kidiplomasia.
Kabla ya uteuzi huo, Mbena alikuwa ofisa mshauri wa ngazi ya kwanza wa Balozi za Vatican pia akihudumu katika Sekretarieti Kuu ya Vatican. Alianza utume wake wa kidiplomasia mwaka 1995, baada ya kupadrishwa mwaka 1992 Jimbo Katoliki la Morogoro.
Katika utumishi wake wa kidiplomasia, Monsinyo amewahi kuhudumu katika nchi mbalimbali ikiwemo Zambia, Panama, Ghana, Trinidad na Tobago, Sudan, Ethiopia, India na Albania. Uzoefu huo wa kimataifa umemwezesha kuwa miongoni mwa wachache wanaopewa nafasi za juu katika mfumo wa utawala wa Vatican.
Ofisi ya Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo, inayojulikana pia kama Ofisi ya Misaada ya Kitume, ina jukumu la kuratibu na kutoa misaada kutoka kwa Papa kwa maskini, walioko pembezoni mwa jamii na waathirika wa majanga makubwa.
Baraza hilo linafanya kazi kwa kushirikiana na mabaraza mengine ya Kipapa kuhakikisha misaada inawafikia walengwa waliokusudiwa.
REPLY HAPA
image quote pre code