Watanzania 147 warejeshwa nchini kutoka Iran, Israel

Watanzania 147 warejeshwa nchini kutoka Iran, Israel

#1

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax amesema mipaka ya nchi ipo salama, na kwamba hali ya ulinzi imeimarishwa.



Dodoma. Watanzania 147 kati ya 663 walioko katika nchi za Iran na Israel wamerejeshwa nchini kutokana na machafuko yaliyoko katika nchi hizo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dennis Londo, ameliambia Bunge leo, Jumatatu, Juni 23, 2025, wakati akijibu hoja za wabunge katika mjadala wa Mpango wa Maendeleo na Bajeti Kuu ya Serikali 2025/26.

Londo amesema Watanzania hao wamerudishwa kutokana na uamuzi wa Serikali, na wapo kwenye mchakato wa kuhakikisha wote wanarudi nchini hadi hali itakapotulia kwenye mataifa hayo.

Amesema kwa sasa dunia ipo katika hali ya sintofahamu kutokana na machafuko yanayoendelea katika nchi hizo, hivyo Rais Samia Suluhu Hassan akatoa maelekezo kwa wizara kwamba iwarudishe watu wake kutoka nchi hizo.

“Tulikuwa na Watanzania 168 nchini Iran na 495 nchini Israel. Mheshimiwa Spika, hadi sasa Serikali imewezesha kurudishwa Watanzania 147, ambapo 42 kutoka Israel na 65 kutoka Iran, wameondoka katika maeneo hayo ya hatari na kuanza safari ya kurejea nchini pamoja na maeneo mengine ya kiusalama,” amesema Londo.

Amebainisha kuwa jitihada hizo zinaratibiwa na wizara kwa kushirikiana na ofisi za ubalozi katika maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Londo, Serikali imeweka mazingira wezeshi ya kuhakikisha wote walioko katika nchi hizo wanarejea nchini wakiwa salama.

Hata hivyo, amesema Tanzania inalaani migogoro inayoendelea katika mataifa hayo, huku ikisisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto kwa njia salama za kidiplomasia na kuzingatia makubaliano ya Umoja wa Kimataifa.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali inafanya mazungumzo na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Tamisemi, ili mikoa na halmashauri zinazopakana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wawezeshwe kushiriki soko la jumuiya hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax, amesema mipaka ya Tanzania ipo salama, na wanaendelea kuimarisha amani na utulivu.

Pia Dk Tax ametangaza neema kwa maofisa na askari kwamba kuanzia Julai mosi, 2025, wataongezewa mafao ili kuendana na mazingira ya sasa na hali ya kiuchumi.

REPLY HAPA


image quote pre code