Watoto 130,000 wazuiwa kupata Masomo yao DRC
Taarifa ya UNICEF iliyotolewa Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri, mashariki wa DRC imesema shule zimeharibiwa, na watoto sasa wamesalia nyumbani.
Zaidi ya shule 290 zimeharibiwa tangu mwanzo wa mwaka huu, na kuwazuia watoto wapatao 130,000 kuhudhuria masomo. Kwa jumla, zaidi ya watoto milioni 1.3 sasa hawahudhurii shule katika jimbo la Ituri pekee.
Watoto wakumbwa na madhila mengi
Kati ya Januari na Aprili 2025, zaidi ya watu 100,000 walilazimika kuhama makazi yao kutokana na ghasia zinazoendelea, nusu yao wakiwa watoto. Katika kipindi hicho hicho, watu wasiopungua 205 waliuawa, huku ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto – ikiwa ni pamoja na utekaji, kukatwa viungo, ukatili wa kingono na utumikishaji wa lazima kwenye vikundi vya kijeshi – ukiongezeka kwa asilimia 32 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
“Tangu mwanzo tumeeleza kuwa mgogoro wa mashariki mwa DRC ni mgogoro wa ulinzi wa watoto,” amesema John Agbor, Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC. “Lakini sasa ni wazi kwamba pia ni janga la elimu. Ghasia na mizozo vinaendelea kuvunja haki ya watoto kujifunza – na kuwafanya kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuingizwa katika makundi ya waasi, kudhulumiwa na kunyanyaswa.”
Zaidi ya watoto milioni 1.8 mashariki mwa DRC hawako shuleni
Mbali na Ituri, majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Tanganyika pia yanakumbwa na changamoto hiyo, ambapo jumla ya watoto zaidi ya milioni 1.8 walioathiriwa na migogoro hawapo shuleni.
REPLY HAPA
image quote pre code