Watu 49 wafariki dunia Afrika Kusini kutokana na mvua kubwa
Maafa makubwa yameripotiwa nchini Afrika Kusini kufuatia mvua kubwa na mafuriko yaliyozikumba sehemu mbalimbali za nchi hiyo.
Idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko sehemu za mashariki mwa Afrika Kusini imeongezeka na kufikia watu 49, wakiwemo watoto 4 katika basi la shule lililosombwa na maji. Haya ni kwa mujibu wa gavana wa mkoa wa Eastern Cape, Lubabalo Oscar Mabuyane.
Katika maeneo mbalimbali ya jimbo la Eastern Cape na KwaZulu-Natal,hali bado ni ya huzuni na taharuki. Idadi ya vifo imepanda hadi kufikia watu 49, huku maafisa wa uokoaji wakihaha kuokoa maisha na kutafuta waathirika katika maporomoko na mito iliyofurika. Oscar Mabuyani ni mkuu wa jimbo la Eastern Cape.
"Tunaendelea kushuhudia ongezeko la idadi ya waliopotea, huku miili mipya ikipatikana na kutambuliwa," alisema Mbuyani.
Watu kupanda juu ya miti
Msemaji wa jimbo la Eastern Cape, Kusewa Ranki,amesema kwamba baadhi ya miili iliyopatikana kutoka Mto Titika ni ya wanafunzi waliokuwa kwenye basi dogo la shule lililosombwa na maji.
Watatu waliokuwa kwenye basi walifanikiwa kuokolewa baada ya kupanda juu ya miti, wakati maji yalipokuwa yakiongezeka.
"Watoto watatu kati yao waliweza kupanda juu ya miti na baadaye wakaokolewa na kikosi chetu cha uokoaji,” alisema Ranki.
Katika jimbo jirani la KwaZulu-Natal, zaidi ya nyumba 80 zimeharibiwa, na takribani watu 277 wameachwa bila makazi. Wengine wamehama kwa hofu ya maporomoko ya ardhi na mafuriko zaidi. Mkazi wa jiji la Durban, Abubakar Umande, anasema hali kwa sasa imeanza kutengemaa, lakini hofu ya mvua zaidi bado imo mioyoni mwa wakazi wengi.
"Kwa sasa hali zetu zinaendelea vizuri isipokuwa kabla ya siku mbili tatu kulikuwa na mvua, sasa leo jua limewaka,” alisema Umande.
Mafuriko yamekuwa yakijirudia
Serikali kuu imetoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari, hasa msimu huu wa baridi kali unaoambatana na athari za hali mbaya ya hewa. Vincent Magwenya ni msemaji mkuu wa serikali.
"Matukio haya na mengine yanaonesha umuhimu wa raia wa Afrika Kusini kuwa waangalifu, kuonesha uangalizi na kushirikiana, wakati athari mbaya zaidi za hali ya hewa ya baridi zikiendelea kushuhudiwa kote nchini,” Magwenya.
Majanga kama haya ya mafuriko na dhoruba yamekuwa yakijirudia kila mwaka katika majimbo ya Eastern Cape na KwaZulu-Natal, yakiacha majeraha ya mwili, kiroho na kijamii kwa maelfu ya watu.
Tayari mamlaka ya hali ya hewa imetoa tahadhari za viwango vya pili na vya nne, ikionya kuhusu mvua ya mawe, upepo mkali, radi, pamoja na mvua kubwa inayoweza kuendelea kuathiri maeneo mbalimbali ya nchi.
REPLY HAPA
image quote pre code