TCU imewaasa wananchi kuepuka kutapeliwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini.
Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la udahili kwa waombaji wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2025/2026.
Taarifa ya Katibu Mkuu wa TCU Prof Charles Kihampa iliyotolewa leo Julai 15, imeeleza kuwa dirisha hilo litakuwa wazi kuanzia leo hadi Agosti 8, 2025 kwa makundi matatu ambayo ni wenye sifa stahiki za kidato cha sita, wenye sifa stahiki za stashahada (Diploma), au sifa linganifu pamoja na wenye sifa stahiki za Cheti cha Awali (Foundation Certificate) cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Prof Kihampa katika taarifa yake amesema Ili kufahamu sifa stahiki kwa makundi matatu yaliyoainisha , vyuo na programu zilizoruhusiwa kudahili, waombaji wanapaswa kusoma vigezo vilivyooneshwa katika vitabu vya mwongozo wa maombi ya udahili vinavyotolewa na TCU (Bachelor’s Degree Admission Guidebooks for 2025/2026 Academic Year) katika tovuti ya TCU (www.tcu.go.tz).
Utaratibu wa kutuma maombi ya udahili
TCU imebainisha kuwa maombi yatumwe moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo mwombaji amevichagua na kuchagua programu za masomo anazozipenda kwa kufuata maelekezo mahususi ya jinsi ya kutuma maombi yanayotolewa na vyuo husika.
Vigezo na sifa za waombaji udahili
Aidha, kwa mujibu wa TCU vigezo na sifa katika programu mbalimbali za masomo vinapatikana katika tovuti za vyuo husika na katika vitabu vya mwongozo wa maombi ya udahili vinavyopatikana katika tovuti ya TCU.
Masuala muhimu ya kuzingatiwa na waombaji
Hata hivyo, waombaji wameshauriwa kusoma kwa makini na kuelewa mwongozo wa udahili uliotolewa na TCU pamoja na maelekezo mahususi ya vyuo kabla ya kuanza kutuma maombi ya udahili.
“Kuingia katika tovuti za vyuo na kuwasiliana na vyuo moja kwa moja ili kujua taratibu za kutuma maombi na kupata taarifa za kina kuhusu programu za masomo ili kujiridhisha kabla ya kutuma maombi, kutuma maombi moja kwa moja vyuoni kupitia mifumo ya kielekroniki iliyowekwa na vyuo husika,” imebainisha taarifa ya Prof Kihampa.
Kihampa amesema waombaji Watanzania wenye vyeti vilivyotolewa na mabaraza ya mitihani nje ya nchi wanapaswa kuwasilisha vyeti vyao katika Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kwa vyeti vya Elimu ya Sekondari au Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa vyeti vya Stashahada ili kupata ithibati ya ulinganifu wa sifa zao kabla ya kutuma maombi ya udahili.
Kwa upande wa waombaji ambao siyo Watanzania, wenye vyeti vilivyotolewa na mabaraza ya mitihani nje ya nchi wanapaswa kutuma maombi ya udahili moja kwa moja kupitia mifumo ya vyuo husika.
“Tume inawahimiza waombaji wote wa udahili kuendelea kupata taarifa sahihi kupitia tovuti ya TCU, tovuti za vyuo vilivyoruhusiwa kudahili wanafunzi wa Shahada ya Kwanza, pamoja na taarifa mbalimbali zinazotolewa na TCU kupitia vyombo vya habari,” amesisitiza Prof Kihampa.
Tahadhari
TCU imetoa wito kwa waombaji wote wa udahili wa shahada ya kwanza kupata ufafanuzi wa suala lolote linalohusu udahili moja kwa moja kwa vyuo husika.
Aidha, iwapo watahitaji maelezo ya jumla wanaweza kuwasiliana na TCU kwa kutumia barua pepe es@tcu.go.tz. Ambapo pia tume imewaasa wananchi kuepuka kutapeliwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini.
REPLY HAPA
image quote pre code