Ajali Mbaya Dodoma Yaua Watatu Baada ya Malori Kugongana na Kuwaka Moto
Watu watatu wamefariki dunia kufuatia ajali mbaya iliyotokea leo asubuhi katika eneo la Mataa, kwenye barabara inayoelekea kwa Dodoma, baada ya magari mawili makubwa kugongana uso kwa uso na kisha kuwaka moto.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Dodoma, Rehema Menda, tukio hilo limetokea majira ya saa 12 asubuhi na kusababisha taharuki kubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Imeelezwa kuwa ajali hiyo ilihusisha lori lenye namba za usajili T179 EQF lililokuwa limebeba mchanga, ambalo lilikuwa likiendeshwa na mtu aliyetambulika kwa jina moja la Lucas. Lori hilo liligongana uso kwa uso na gari jingine lenye namba T764 EPW pamoja na tela namba T238 EPW, lililokuwa limebeba saruji likitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma.
Baada ya kugongana, magari hayo yaliteketea kwa moto uliodaiwa kusababishwa na msuguano mkali uliotokea wakati wa ajali. Askari wa zimamoto waliofika eneo la tukio walifanya juhudi za kuuzima moto na kuokoa miili ya watu watatu waliopoteza maisha.
Hadi sasa, mtu aliyethibitishwa kutambulika ni dereva wa lori la mchanga, Lucas, huku utambuzi wa wengine ukiendelea kufanywa na vyombo husika.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Emanuel, amesema watu waliokuwa kwenye gari lililobeba saruji walifanikiwa kutoka salama mara baada ya ajali. Hata hivyo, waliokuwa ndani ya lori la mchanga walikwama baada ya mlango kugoma kufunguka hadi askari wa uokozi walipofika na kuuvunja.
Ajali hiyo imeibua maswali mapya kuhusu usalama wa vyombo vikubwa barabarani, hasa katika maeneo yenye msongamano wa magari makubwa yanayosafirisha mizigo kati ya Dar es Salaam na Dodoma.
Mamlaka husika zinaendelea kuchunguza chanzo halisi cha ajali hiyo.
You, Mehreen and others


