China Yaweka Historia Mpya Angani, Mwanaanga Ataishi Mwaka Mzima Kwenye Kituo cha Tiangong
China imeandika historia mpya katika sekta ya anga baada ya kuzindua misheni mpya ya watu watatu kuelekea kituo chake cha anga cha Tiangong Space Station, huku mmoja wa wanaanga akitarajiwa kuishi angani kwa mwaka mzima.
Misheni hiyo inayojulikana kama Shenzhou-23 ilizinduliwa rasmi Jumapili kwa kutumia roketi ya Long March 2F kutoka kituo cha kurushia vyombo vya anga cha Jiuquan kilichopo katika Jangwa la Gobi, kaskazini magharibi mwa China.
Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya China katika mpango wake mkubwa wa kupeleka binadamu Mwezini ifikapo mwaka 2030.
Kwa zaidi ya miaka 30 sasa, China imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika teknolojia ya anga kwa lengo la kuwa moja ya mataifa yenye nguvu zaidi katika uchunguzi wa anga za juu duniani.
Tofauti na misheni zilizopita ambazo wanaanga walikaa kwa miezi sita pekee katika kituo cha Tiangong, safari hii inaleta rekodi mpya ambapo mwanaanga mmoja ataendelea kubaki katika mzunguko wa Dunia kwa muda wa mwaka mmoja mzima.
Miongoni mwa wanaanga waliopo katika safari hiyo ni Li Jiaying mwenye umri wa miaka 43 ambaye ameweka historia kuwa mwanaanga wa kwanza kutoka Hong Kong kushiriki katika misheni ya anga ya China. Kabla ya kujiunga na mpango huo, Li aliwahi kufanya kazi katika jeshi la polisi la Hong Kong.
Wengine waliopo kwenye misheni hiyo ni Zhu Yangzhu mwenye umri wa miaka 39 ambaye ni mhandisi wa anga pamoja na Zhang Zhiyuan aliyewahi kuwa rubani wa Jeshi la Anga la China. Kwa wote wawili, hii ni safari yao ya kwanza kwenda angani.
Wakiwa ndani ya kituo cha Tiangong, wanaanga hao wanatarajiwa kufanya tafiti mbalimbali za kisayansi zinazohusisha sayansi ya maisha, tiba, fizikia ya vimiminika pamoja na sayansi ya vifaa.
Jaribio kubwa zaidi katika misheni hiyo ni kuchunguza athari za kuishi kwa muda mrefu katika mazingira yenye mvutano mdogo wa nguvu za uvutano. Utafiti huo unatarajiwa kusaidia maandalizi ya safari za baadaye kuelekea Mwezini na hata sayari ya Mirihi.
Shirika la anga la China limesema jina la mwanaanga atakayebaki angani kwa mwaka mmoja litatangazwa baadaye kulingana na maendeleo ya misheni hiyo.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa unajimu kutoka Chuo Kikuu cha Macquarie nchini Australia, Richard de Grijs, safari za muda mrefu angani bado zina changamoto kubwa ikiwemo kupungua kwa nguvu za mifupa na misuli, madhara ya mionzi ya anga, matatizo ya usingizi pamoja na uchovu wa kisaikolojia.
Aidha amesema maendeleo ya mifumo ya kuchakata maji, hewa na huduma za dharura za kiafya yatakuwa muhimu sana katika kuhakikisha mafanikio ya safari ndefu za anga katika miaka ijayo.





Post a Comment
Related Discussions...