Ferrari Yazindua Gari Lake la Kwanza la Umeme lenye Thamani ya Zaidi ya Bilioni 1.6 za Kitanzania
Kampuni maarufu ya kutengeneza magari ya kifahari ya Italia, Ferrari, imezindua rasmi gari lake la kwanza kabisa linalotumia umeme kwa asilimia 100, hatua inayotajwa kuwa ya kihistoria katika ulimwengu wa magari ya kifahari.
Gari hilo jipya linaloitwa Luce, ambalo kwa lugha ya Kiitaliano linamaanisha “mwanga”, lina thamani ya euro 550,000 sawa na dola 640,000 za Marekani, kiasi kinachokadiriwa kuzidi Shilingi Bilioni 1.6 za Kitanzania.
Tofauti na magari mengi ya kawaida ya Ferrari yenye muundo wa michezo kwa watu wawili, Luce ni gari lenye milango minne na uwezo wa kubeba watu watano, jambo linalolifanya kuwa chaguo jipya kwa familia tajiri zinazopenda anasa na teknolojia ya kisasa.
Ferrari imesema maendeleo ya gari hilo yalichukua zaidi ya miaka mitano, huku likibuniwa kwa ushirikiano na mbunifu maarufu wa zamani wa kampuni ya Apple, Jony Ive, kupitia kundi lake la ubunifu la LoveFrom.
Mkurugenzi Mkuu wa Ferrari, Benedetto Vigna, amesema gari hilo linaonyesha mwelekeo mpya wa kampuni hiyo katika dunia ya teknolojia ya magari ya umeme.
Luce lina injini nne za umeme, kila gurudumu likiwa na motor yake maalum, jambo linalolipa uwezo wa kuzalisha zaidi ya farasi 1,000 wa nguvu, huku likifikia kasi ya zaidi ya kilomita 310 kwa saa.
Pamoja na uzito unaozidi tani 2.2, Ferrari imesema gari hilo lina uwezo wa kusafiri zaidi ya kilomita 500 kabla ya kuhitaji kuchajiwa tena.
Katika uzinduzi wake uliofanyika jijini Rome, Italia, Ferrari ilionyesha magari matano ya Luce yenye rangi tofauti kuanzia nyekundu maarufu ya Ferrari hadi nyeupe na bluu hafifu, yakionyesha muonekano mpya tofauti na magari yao ya zamani yaliyokuwa na sura kali na ya kimichezo zaidi.
Ndani ya gari hilo, Ferrari imechanganya anasa za kawaida kama ngozi, vioo na alumini maalum pamoja na teknolojia ya kisasa, huku ikiweka baadhi ya vitufe vya kawaida badala ya kutegemea mfumo wa kugusa pekee kama ilivyo kwa baadhi ya magari ya umeme ya kampuni ya Tesla na wazalishaji wengine kutoka China.
Ferrari inaamini kuwa Luce litawavutia wateja wapya hasa katika masoko makubwa kama China ambako matumizi ya magari ya umeme yanaongezeka kwa kasi huku magari makubwa ya mafuta yakitozwa kodi kubwa.





Post a Comment
Related Discussions...