Hali ya majeraha ya Lionel Messi wiki chache kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia 2026.
Kocha wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Scaloni, ametoa taarifa kuhusu hali ya majeraha ya nahodha wake Lionel Messi huku zikiwa zimesalia wiki chache kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia 2026.
Scaloni amesema bado kuna wasiwasi kuhusu utimamu wa baadhi ya wachezaji wa Argentina, akiwemo Messi, wakati akijiandaa kutangaza kikosi chake cha mwisho cha wachezaji 26 watakaoshiriki mashindano hayo makubwa duniani.
Hofu kuhusu hali ya Messi ilianza baada ya mshambuliaji huyo kuomba kutolewa nje katika dakika ya 73 wakati klabu yake ya Inter Miami CF ilipoibuka na ushindi wa mabao 6-4 dhidi ya Philadelphia Union. Tukio hilo liliibua hofu kubwa kwa mashabiki kuhusu uwezekano wa Messi kuukosa michuano ya Kombe la Dunia.
Baadaye, Inter Miami ilitoa taarifa ya kitabibu ikieleza kuwa Messi alipata uchovu wa misuli katika sehemu ya nyuma ya paja la kushoto (hamstring), hali iliyotokana na mzigo mkubwa wa mechi.
“Baada ya vipimo vya ziada vya kitabibu vilivyofanywa Jumatatu, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kuna uchovu mkubwa wa misuli ya nyuma ya paja la kushoto. Muda wa kurejea kwake uwanjani utategemea maendeleo ya afya yake na namna atakavyopona,” ilisema taarifa hiyo.
Akizungumza na DSports kuhusu hali ya Messi, Scaloni alisema taarifa za awali hazionyeshi hali mbaya sana, lakini bado wanahitaji kusubiri majibu ya vipimo zaidi.
“Taarifa za mwanzo si mbaya sana; tunahitaji kusubiri kuona maendeleo yake pamoja na majibu ya vipimo zaidi ili kuthibitisha tathmini ya kwanza ya madaktari,” alisema Scaloni.
Hata hivyo, kocha huyo alikiri kuwa mshindi huyo wa Ballon d’Or mara nane hatajiunga na kambi ya maandalizi akiwa katika kiwango chake bora cha utimamu wa mwili.
Scaloni pia alifichua kuwa Messi si mchezaji pekee anayekabiliana na changamoto ya majeraha kuelekea Kombe la Dunia.
“Sote tulitamani Messi aje kambini akiwa fiti kabisa, lakini hali si hivyo. Sio yeye pekee, kuna wachezaji wengine kadhaa ambao bado wanaendelea kupona majeraha yao. Kipaumbele chetu sasa ni kuhakikisha wanapona vizuri ili wafike Kombe la Dunia wakiwa katika hali bora,” aliongeza Scaloni.
Argentina, mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia, wanakabiliwa na presha ya kuhakikisha nyota wao huyo anarejea katika ubora wake kabla ya kuanza kwa mashindano hayo. Katika hatua ya makundi, Argentina imepangwa Kundi J pamoja na Algeria, Austria na Jordan.





Post a Comment
Related Discussions...