Harry Maguire hatajumuishwa kwenye kikosi cha England kitakachoshiriki Kombe la Dunia 2026

Beki wa klabu ya Manchester United na timu ya taifa ya England, Harry Maguire, ameweka wazi kuwa hatajumuishwa kwenye kikosi cha England kitakachoshiriki Kombe la Dunia 2026.

Kocha wa England, Thomas Tuchel, anatarajiwa kutangaza rasmi kikosi cha wachezaji 26 siku ya Ijumaa, Mei 22, lakini Maguire hatakuwa sehemu ya safari ya kuelekea Marekani, Mexico na Canada kwa ajili ya michuano hiyo mikubwa ya dunia.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, Tuchel aliwapigia simu baadhi ya wachezaji siku ya Alhamisi kuwajulisha kuwa hawakufanikiwa kuingia kwenye kikosi cha mwisho cha England, ambayo ipo Kundi L pamoja na Croatia, Ghana na Panama.

Maguire mwenye umri wa miaka 33, ambaye ameichezea England mara 66, ameonyesha kusikitishwa sana na uamuzi huo kupitia ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

“Niliamini ningekuwa sehemu muhimu ya timu ya taifa majira haya kutokana na kiwango nilichoonyesha msimu huu. Nimeshtushwa na nimeumia sana kwa uamuzi huu,” aliandika Maguire.

Aliendelea kusema kuwa kuvaa jezi ya England imekuwa moja ya heshima kubwa kwake katika maisha yake ya soka, huku akiwaombea kila la heri wachezaji watakaoiwakilisha nchi hiyo kwenye mashindano hayo.

Maguire alikuwa ameanza kurejea kwenye kiwango bora ndani ya Manchester United chini ya kocha Michael Carrick katika nusu ya pili ya msimu wa Ligi Kuu England.

Tangu Carrick alipoanza kuinoa timu hiyo Januari 17, Maguire amekosa michezo miwili pekee ya ligi na amecheza dakika zote 90 katika mechi nyingi, akiwa nguzo muhimu ya safu ya ulinzi ya United.

Kiwango chake kizuri kilisaidia Manchester United kufuzu kushiriki michuano ya UEFA Champions League msimu ujao, jambo lililowafanya wengi kuamini angeitwa tena kwenye kikosi cha taifa kabla ya kuachwa nje kwa mshangao mkubwa.

...See more

DISCUSSIONS BOX(MAONI)|REPLY

Related Discussions...