Madhara ya Acid Reflux (GERD) Yanayopaswa Kujulikana
Acid Reflux au GERD (Gastroesophageal Reflux Disease) ni hali ambapo tindikali kutoka tumboni hupanda kwenda kwenye umio mara kwa mara. Madaktari kutoka taasisi kubwa za afya duniani wanaeleza kuwa hali hii ikipuuzwa inaweza kuleta madhara makubwa kwa muda mrefu.
1. Kuungua na Kuvimba kwa Umio (Esophagitis)
Tindikali inapopanda mara kwa mara, huunguza ukuta wa umio na kusababisha maumivu, kuungua kifuani, na wakati mwingine vidonda. Watu wengi huanza kwa kuhisi “kiungulia” lakini baadaye huanza kupata maumivu makali wakati wa kumeza chakula.
Daktari wa mfumo wa chakula kutoka Cleveland Clinic alieleza kuwa:
“GERD inaweza kusababisha uvimbe wa umio na hata vidonda ikiwa haitatibiwa mapema.”
2. Kupata Ugumu wa Kumeza Chakula
Kwa mujibu wa Mayo Clinic, tindikali inaweza kuacha makovu ndani ya umio. Makovu hayo hupunguza njia ya chakula kupita na kufanya mgonjwa ashindwe kumeza vizuri. Wengine huhisi chakula kinakwamia kooni au kifuani.
Baadhi ya wagonjwa wameeleza kuwa walikuwa wakihisi hata maji yanapita kwa shida kutokana na uharibifu wa muda mrefu wa GERD.
3. Koo Kuwasha na Kikohozi Kisichoisha
Acid Reflux haiishii tumboni pekee. Tindikali inaweza kufika kooni na kwenye njia ya hewa na kusababisha:
- Koo kuwasha
- Kukauka sauti
- Kikohozi cha muda mrefu
- Harufu mbaya mdomoni
- Kupumua kwa shida hasa usiku
Madaktari wanasema watu wengine hudhani wana mafua au asthma, kumbe chanzo ni GERD.
4. Matatizo ya Usingizi
Wagonjwa wengi wa Acid Reflux hulalamika kushindwa kulala vizuri kwa sababu tindikali hupanda zaidi wanapolala chali. Wengine huamka usiku wakikohoa au wakihisi kama wanakabwa.
Mgonjwa mmoja kwenye mjadala wa GERD alisema:
“Nilikuwa naamka usiku nikikabwa na tindikali hadi kushindwa kulala vizuri kwa miaka mingi.”
5. Barrett’s Esophagus — Hatari ya Saratani
Hili ni moja ya madhara makubwa zaidi. Mayo Clinic inaeleza kuwa tindikali ya muda mrefu inaweza kubadilisha seli za umio na kusababisha hali inayoitwa Barrett’s Esophagus, ambayo huongeza hatari ya kupata saratani ya umio.
Baadhi ya wagonjwa waliopuuza GERD kwa miaka mingi walikuja kugundulika na hatua za awali za saratani baada ya kupata Barrett’s Esophagus.
6. Maumivu ya Kifua Yanayofanana na Tatizo la Moyo
GERD inaweza kusababisha maumivu makali ya kifua kiasi kwamba mtu anaweza kudhani ana shida ya moyo. Afyaclass inaonya kuwa maumivu hayo yanaweza kufanana sana na dalili za mshtuko wa moyo.
7. Athari za Kisaikolojia na Maisha ya Kila Siku
Watu wengi wenye GERD ya muda mrefu hupata:
- Wasiwasi
- Stress
- Kukosa usingizi
- Kupungua uzito
- Hofu ya kula baadhi ya vyakula
Baadhi ya wagonjwa wameeleza kuwa walilazimika kubadilisha kabisa maisha yao kwa kuacha vyakula vya mafuta, soda, kahawa, pombe, na kula usiku.
Dalili Zinazopaswa Kukufanya Umwone Daktari Haraka
Muone daktari ikiwa:
- Kiungulia kinatokea mara nyingi kila wiki
- Unashindwa kumeza vizuri
- Unatapika damu
- Unapungua uzito bila sababu
- Una maumivu makali ya kifua
- Kikohozi au sauti ya kukauka haviishi
Namna ya Kupunguza Acid Reflux
Madaktari wa Afyaclass,Mayo Clinic na Cleveland Clinic wanashauri:
- Epuka kula usiku sana
- Punguza vyakula vya mafuta na pilipili nyingi
- Epuka kulala mara baada ya kula
- Punguza uzito kama una uzito mkubwa
- Acha sigara na pombe
- Lala ukiwa umeinua kichwa kidogo
- Tumia dawa kwa ushauri wa daktari


.jpeg)



Post a Comment
Related Discussions...