Maduka ya Wafanyabiashara wa Kigeni Yaporwa Afrika Kusini Kufuatia Mvutano wa Kijamii

Mvutano kati ya wakazi wa eneo la Estcourt katika jimbo la KwaZulu-Natal, Afrika Kusini, umechukua sura mpya baada ya maduka kadhaa yanayomilikiwa na raia wa kigeni kuvamiwa na kuporwa na wananchi.

Tukio hilo lilitokea asubuhi ya Ijumaa, Mei 29, ambapo maduka sita yanayomilikiwa na wafanyabiashara wa kigeni yalilengwa na kundi la watu waliokuwa na hasira kutokana na mgogoro unaohusisha uendeshaji wa biashara za wageni katika eneo hilo.

Msemaji wa polisi wa jimbo hilo, Luteni Kanali Robert Netshiunda, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa hali ya usalama imedhibitiwa, huku hakuna taarifa za majeruhi zilizoripotiwa.

Kwa mujibu wa polisi, vurugu hizo zinaaminika kuhusishwa na uamuzi wa baadhi ya wafanyabiashara wa kigeni kufungua kesi mahakamani dhidi ya Meya wa eneo hilo, Mduduzi Myeza. Meya huyo alikuwa ametoa agizo lililowataka wafanyabiashara wa kigeni ambao hawana nyaraka halali za uhamiaji kuondoka mjini humo ndani ya siku 21.

Muda wa agizo hilo ulimalizika Mei 27, huku wafanyabiashara waliolalamika wakipeleka suala hilo mahakamani siku chache kabla ya muda huo kuisha. Hatua hiyo imeonekana kuzidisha mvutano kati ya wenyeji na wageni wanaofanya biashara katika eneo hilo.

Polisi wameeleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini waliohusika na uporaji huo, huku ulinzi ukiimarishwa ili kuzuia matukio mengine ya fujo. Aidha, mamlaka za eneo hilo zimeandaa kikao maalumu kitakachowakutanisha viongozi wa serikali za mitaa, polisi na wamiliki wa jengo lililokuwa na maduka yaliyoathirika.

Lengo la kikao hicho ni kutafuta suluhisho la kudumu kwa mvutano unaoendelea kati ya wakazi wa eneo hilo, wafanyabiashara wa kigeni na viongozi wa serikali.

Tukio hili linaongeza wasiwasi kuhusu usalama wa raia wa kigeni nchini Afrika Kusini, ambako mara kadhaa kumeshuhudiwa migogoro inayohusishwa na ushindani wa kiuchumi, ajira na biashara kati ya wenyeji na wahamiaji kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

...See more

Una maoni gani? Changia hapa!

Mijadala Inayoendelea