Mahakama ya Kenya Yasitisha Mpango wa Kituo cha Karantini ya Ebola
Mahakama ya Kenya imetoa amri ya muda inayositisha mpango wa kuanzisha kituo cha karantini ya Ebola kinachodaiwa kuhusishwa na Marekani, huku ikiizuia serikali kuruhusu kuingia nchini kwa watu walioambukizwa virusi hivyo hadi kesi iliyofunguliwa na taasisi ya Katiba Institute itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Uamuzi huo umetolewa saa chache baada ya mahakama kupokea na kuthibitisha kuwa ombi la Katiba Institute ni la dharura. Taasisi hiyo inapinga kile inachodai kuwa ni makubaliano kati ya Kenya na baadhi ya mataifa ya kigeni, yakiwemo Marekani, kuhusu usimamizi wa visa vya Ebola na uwezekano wa wagonjwa hao kutibiwa nchini Kenya.
Katika amri yake, mahakama imeeleza kuwa hatua zote zinazohusiana na kuanzishwa kwa vituo vya karantini, kutenga wagonjwa au matibabu maalum ya Ebola zitasimamishwa hadi pande zote zitakapopewa nafasi ya kusikilizwa.
Mahakama pia imeagiza mlalamikaji kuwasilisha nyaraka zote za kesi kwa washtakiwa ndani ya saa 24, huku washtakiwa wakitakiwa kuwasilisha majibu yao ndani ya saa 48 baada ya kupokea hati hizo. Kesi hiyo inatarajiwa kurejea mahakamani kwa maelekezo zaidi baada ya taratibu hizo kukamilika.
Amri hizo za muda zinamaanisha kuwa serikali ya Kenya haiwezi kwa sasa kuendelea na mipango yoyote inayohusisha kupokea au kutibu watu walioambukizwa Ebola chini ya mpango unaopingwa mahakamani.
Hatua hiyo imeibuka wakati Marekani ikitangaza msaada wa dola milioni 13.5 kwa Kenya kwa ajili ya kuimarisha maandalizi dhidi ya Ebola. Msaada huo ni sehemu ya juhudi za ushirikiano kati ya Nairobi na Washington katika kukabiliana na tishio la mlipuko wa Ebola unaoendelea katika ukanda huo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka upande wa Marekani, mazungumzo yalifanyika kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, na Rais wa Kenya, William Ruto, yakilenga kuimarisha uwezo wa Kenya wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko pamoja na upatikanaji wa vifaa muhimu vya afya.
Wakati mjadala wa afya ya umma ukiendelea, uamuzi wa mahakama sasa unaweka mwelekeo mpya katika suala hilo, huku wananchi na wadau mbalimbali wakisubiri kusikia uamuzi wa mwisho kuhusu uhalali wa mpango huo na nafasi ya Kenya katika juhudi za kikanda za kukabiliana na Ebola.




Post a Comment