Jamii ya Inchanga, mkoani KwaZulu-Natal nchini South Africa imekumbwa na mshtuko mkubwa baada ya mfamasia kijana, Nomzila Madinane, kuuawa kwa kupigwa risasi siku chache tu baada ya kufungua duka lake la dawa kwa lengo la kuwasaidia wakazi kupata huduma za afya karibu zaidi.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Jumanne, Mei 19, 2026, ndani ya duka hilo jipya la dawa ambapo watu wenye silaha walivamia na kufyatua risasi hovyo. Mbali na Nomzila kupoteza maisha, mfanyakazi mmoja wa kike aliyekuwa cashier pamoja na mlinzi wa duka hilo pia walifariki kutokana na shambulio hilo.

Kwa mujibu wa polisi wa KwaZulu-Natal, kesi tatu za mauaji zimefunguliwa kufuatia tukio hilo la kutisha. Polisi walisema washambuliaji hao walikuwa wanaume watatu wenye silaha waliovamia ghafla na kuanza kufyatua risasi.

Msemaji wa polisi, Robert Netshiunda, alisema kuwa wahanga hao walishambuliwa wakiwa ndani ya duka hilo, huku mlinzi akijeruhiwa vibaya alipokuwa akijaribu kuzuia shambulio hilo kabla ya kufariki hospitalini.

Taarifa zinaeleza kuwa Nomzila Madinane alikuwa ameanzisha duka hilo la dawa baada ya kuona changamoto kubwa iliyokuwepo katika eneo hilo, ambapo wakazi wengi walilazimika kusafiri umbali mrefu kupata dawa na huduma za afya. Hatua yake ilionekana kama matumaini mapya kwa jamii ya Inchanga.

Wananchi wengi wameeleza huzuni yao wakimtaja Nomzila kama kijana mwenye maono, aliyejitolea kusaidia jamii yake kupitia taaluma yake ya famasia. Kifo chake kimeacha simanzi kubwa kwa familia, marafiki na wakazi wa eneo hilo.

Hadi sasa, chanzo cha shambulio hilo bado hakijafahamika rasmi. Polisi wanaendelea na uchunguzi kubaini kama tukio hilo lilihusishwa na ujambazi au sababu nyingine.




...See more

DISCUSSIONS BOX(MAONI)|REPLY

Related Discussions...