Michael Carrick Karibu Kutangazwa Kocha Mkuu wa Kudumu Manchester United
Klabu ya Manchester United ipo hatua za mwisho za kumthibitisha Michael Carrick kuwa kocha mkuu wa kudumu baada ya kufikia makubaliano ya awali ya mkataba mpya wa miaka miwili.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, mazungumzo kati ya Carrick na uongozi wa klabu yanaendelea vizuri huku mkataba wake wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu. Mpango uliopo ni kumpa mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.
Carrick mwenye umri wa miaka 44 ameonyesha mafanikio makubwa tangu alipopewa jukumu la kuinoa United kwa muda. Katika michezo 15 ya Ligi Kuu England aliyosimamia, ameiongoza timu hiyo kushinda michezo 10, jambo ambalo limewavutia viongozi wa juu wa klabu hiyo.
Uongozi wa soka ndani ya Manchester United unadaiwa kupendekeza rasmi Carrick apewe nafasi hiyo ya kudumu kutokana na kiwango kizuri cha timu chini yake. Afisa Mkuu Mtendaji wa klabu, Omar Berrada pamoja na mkurugenzi wa soka Jason Wilcox wanaelezwa kufurahishwa na kazi yake na kutaka aendelee kubaki Old Trafford.
Mbali na Carrick, klabu hiyo pia ipo kwenye mazungumzo ya kuongeza mikataba ya benchi lake la ufundi. Wanaotarajiwa kuendelea kubaki ni Steve Holland, Jonathan Woodgate, Jonny Evans pamoja na Travis Binnion.
Akizungumza kuhusu mustakabali wake, Carrick alisema hali itakuwa wazi hivi karibuni, huku akieleza fahari yake kurejea Manchester United kama kocha baada ya kuitumikia klabu hiyo zamani akiwa mchezaji.
Carrick amesema kurejea kwenye michuano ya UEFA Champions League ni hatua kubwa kwa timu hiyo, na amepongeza juhudi za wachezaji pamoja na sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki.
Kocha huyo pia amesisitiza umuhimu wa mashabiki wa Manchester United, akisema wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya timu katika miezi ya hivi karibuni na kwamba ataendelea kuwashukuru kwa sapoti yao kubwa ndani na nje ya uwanja.





Post a Comment
Related Discussions...