Moto mkubwa wateketeza bweni la wanafunzi katika Chuo cha Wasichana eneo la Gilgil Kenya

Hofu imetanda katika Kaunti ya Nakuru nchini Kenya baada ya moto mkubwa kuteketeza bweni la wanafunzi katika Chuo cha Wasichana Utumishi kilichopo eneo la Gilgil, huku taarifa za awali zikieleza kuwa baadhi ya wanafunzi huenda wamepoteza maisha.

Kwa mujibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu Kenya, moto huo ulizuka majira ya saa saba usiku wa kuamkia Alhamisi na kuripotiwa rasmi takriban saa tisa na nusu usiku. Mara baada ya taarifa hiyo kupokelewa, vikosi vya uokoaji vilitumwa haraka katika eneo hilo kuanza operesheni za dharura.

Kupitia taarifa rasmi, Msalaba Mwekundu Kenya ulisema wahudumu wa kwanza, timu ya ambulensi ya EMS Kenya pamoja na wataalamu wa usaidizi wa kisaikolojia wamewekwa eneo la tukio kusaidia wanafunzi walioathirika na kushirikiana na mamlaka nyingine katika juhudi za uokoaji.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Bonde la Ufa, Samuel Ndanyi, amesema bado kuna wanafunzi wasiopungua kumi ambao hawajulikani walipo huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha moto huo na idadi kamili ya walioathirika.

“Timu zetu zinaendelea kukusanya taarifa zaidi na kuwabaini wanafunzi wote waliokuwa bweni wakati wa tukio. Kuna taarifa za vifo na ni muhimu familia ziarifiwe kwanza kabla ya kutoa taarifa kamili kwa umma,” alisema Ndanyi.

Tukio hilo limewaibua hofu kubwa wazazi na wananchi wa Gilgil pamoja na maeneo ya jirani, ambapo mamia walikusanyika nje ya lango la shule kutafuta taarifa kuhusu watoto wao. Polisi walilazimika kuimarisha ulinzi na kuruhusu wazazi pekee kuingia ndani ya shule wakati shughuli za uokoaji zikiendelea.

Wanafunzi waliojeruhiwa wamepelekwa katika Hospitali ya St. Joseph’s Gilgil kwa matibabu na uchunguzi zaidi huku mamlaka zikiahidi kutoa taarifa kamili baada ya operesheni ya uokoaji na uchunguzi kukamilika.

Tukio hilo limezua majonzi makubwa nchini Kenya, huku wengi wakitaka uchunguzi wa kina ufanyike kubaini chanzo cha moto huo na hatua zaidi kuchukuliwa kuimarisha usalama katika mabweni ya shule.

...See more

WEKA COMMENT YAKO HAPA(MAONI)KUHUSU MADA HII

Related Discussions...