Uliza / Post Makala (New Post)

Preview
Imepokelewa!

Asante sana. Posti yako imetumwa kikamilifu na kwa sasa ipo under review. Itafanyiwa kazi na kuonekana hivi punde.

Mwanamke Aliyenusurika Mashambulizi ya 9/11 Asema Mwili Wake Unachoma Kutoka Ndani

Mwanamke mmoja kutoka jimbo la Arizona nchini Marekani, Jenn Ashcraft, ambaye alinusurika mashambulizi mawili makubwa yaliyotokea katika majengo ya World Trade Center jijini New York, amesema sasa anakabiliwa na ugonjwa mkali unaoufanya mwili wake “kujichoma kutoka ndani kwenda nje.”

Ashcraft mwenye umri wa miaka 60 amesema kumbukumbu za matukio hayo bado zinamtesa huku akiwa amelazwa hospitalini akipambana na hali mbaya ya kiafya ambayo imebadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa.

Jenn alikuwa ndani ya eneo la World Trade Center mwaka 1993 wakati bomu lililipuka chini ya jengo la North Tower katika shambulizi la kwanza dhidi ya majengo hayo.

“Nilihisi mlipuko huo. Nilihisi mwili wangu ukitikisika kabisa,” alisema Ashcraft akielezea tukio hilo la kutisha.

Miaka kadhaa baadaye, Septemba 11 mwaka 2001, alijikuta tena karibu na majengo hayo wakati ndege zilipoelekezwa na magaidi na kugonga minara ya World Trade Center katika moja ya mashambulizi mabaya zaidi kuwahi kutokea Marekani.

“Nilikuwa natembea kuelekea kwenye majengo hayo. Niliona ndege ya kwanza ikigonga,” alisema.

Baada ya matukio hayo, Ashcraft alihamia Prescott, Arizona ambako alianza kujitolea katika shughuli za kama njia ya kuponya majeraha ya kihisia na kuwaheshimu wazima moto waliopoteza maisha yao wakati wa mashambulizi ya 9/11.

Kupitia shughuli hizo za kujitolea, alimfahamu mume wake Tom Ashcraft, ambaye mwanawe alikuwa miongoni mwa wazima moto 19 wa kikosi cha Granite Mountain Hotshots waliokufa wakipambana na moto mkubwa wa Yarnell Hill mwaka 2013.

Ashcraft amesema kwa miaka mingi alikuwa akiratibu kampeni za uchangiaji damu na pia kutoa damu kusaidia wengine, lakini sasa yeye ndiye anayehitaji msaada huo.

Kwa mujibu wake, alianza kupata matatizo ya kiafya kwa muda mrefu tangu baada ya mashambulizi hayo, lakini hali yake ilibadilika ghafla wiki za hivi karibuni.

“Ngozi yangu ilianza kuvuja damu kwenye kucha, na mwili wangu ukaanza kujishambulia wenyewe,” alisema.

Madaktari walimthibitishia kuwa ana ugonjwa wa kinga ya mwili kushambulia mwili wenyewe, maarufu kama autoimmune disorder. Ashcraft anaeleza hali hiyo kama mwili wake “kuwaka moto kutoka ndani.”

“Maumivu yapo kifuani, mgongoni, usoni, mikononi na miguuni. Ni maumivu makali sana,” alisema.

Madaktari sasa wanampa matibabu ya kuongeza kingamwili kwa lengo la kuokoa maisha yake.

Hata hivyo, programu maalumu ya afya ya manusura wa mashambulizi ya 9/11 ya World Trade Center bado haitambui rasmi magonjwa ya autoimmune kama sehemu ya madhara yanayotokana na mashambulizi hayo, jambo ambalo limezua mijadala na maombi ya kuongeza magonjwa hayo kwenye orodha ya magonjwa yanayostahili msaada.

Ashcraft amesema anatamani simulizi yake iwe sauti ya manusura wengine wengi wanaoendelea kuteseka kimya kimya kutokana na madhara ya muda mrefu ya majanga hayo.

“Hatupaswi kupitia haya peke yetu,” alisema.

...See more

DISCUSSIONS BOX(MAONI)|REPLY

Related Discussions...