Ongezeko kubwa la bei ya mafuta Kenya na Mgomo wa Wahudumu wa Matatu

Sekta ya uchukuzi nchini Kenya imeingia katika hali ya sintofahamu baada ya wahudumu wa magari ya uchukuzi maarufu kama matatu kutangaza mgomo wa kitaifa utakaonza siku ya Jumatatu, wakipinga ongezeko kubwa la bei ya mafuta ambalo limeendelea kuwa mzigo kwa wamiliki wa magari na wananchi kwa ujumla.

Hatua hiyo imekuja sambamba na ongezeko la nauli kwa asilimia 50, jambo ambalo tayari limeanza kuwaumiza wananchi wengi wanaotegemea matatu kwa shughuli zao za kila siku. Abiria katika miji mbalimbali, hususan Nairobi, wameeleza wasiwasi wao kuhusu kupanda kwa gharama za usafiri huku hali ya maisha ikiendelea kuwa ngumu kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu.

Chama cha Wamiliki wa Matatu nchini Kenya kimesema kuwa sekta hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto kubwa kutokana na gharama za mafuta kupanda kwa kasi. Kwa mujibu wa chama hicho, gharama za uendeshaji zimeongezeka kupita kiwango kinachoweza kuvumilika, hali inayowalazimu kuongeza nauli ili kuendelea kutoa huduma.

Viongozi wa sekta hiyo wameionya serikali ya Kenya kuwa iwapo hakutakuwa na hatua za haraka kushughulikia malalamiko yao, shughuli za uchukuzi zinaweza kusimama kabisa. Wamesema kuwa kupanda kwa bei ya mafuta kunaathiri moja kwa moja mapato yao pamoja na uwezo wa wananchi kumudu nauli mpya.

Ongezeko hilo la nauli limeanza kutekelezwa mara moja kufuatia hatua ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati nchini Kenya (EPRA) kuongeza bei ya mafuta siku chache zilizopita. Kwa sasa mjini Nairobi, bei ya petroli imefikia Sh214.25 huku dizeli ikiuzwa kwa Sh242.92, hali ambayo imezua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi na wadau wa uchumi.

Wakenya wengi sasa wana hofu kuwa mgomo huo unaweza kusababisha usumbufu mkubwa wa usafiri katika maeneo mbalimbali ya nchi, hasa kwa wafanyakazi, wanafunzi na wafanyabiashara wanaotegemea huduma za matatu kila siku. Serikali ya Kenya inatarajiwa kutoa msimamo wake huku wananchi wakisubiri kuona kama kutakuwa na suluhisho kabla ya mgomo huo kuanza rasmi.

...See more

DISCUSSIONS BOX(MAONI)|REPLY

Related Discussions...