Polisi wajigeuza wacheza shoo wenye mvuto ili kumnasa muuzaji wa dawa za kulevya

Kikosi cha polisi nchini Thailand kimezua gumzo mitandaoni baada ya maafisa wake kujibadilisha na kuvaa kama wacheza shoo wanawake wenye mvuto ili kumkamata muuzaji wa dawa za kulevya aliyekuwa akisakwa kwa muda.

Kikosi hicho kilichokuwa na polisi watano wanaume pamoja na askari mmoja mwanamke kilichapisha picha kwenye Facebook kikionyesha maafisa hao wakiwa wamevalia magauni na kutabasamu baada ya kufanikisha operesheni hiyo katika tamasha la dansi za mitaani lililofanyika mkoani Lopburi, Thailand.

Mshukiwa huyo anayejulikana kwa jina la Mekha Fa-wap-wap alikamatwa akiwa na vidonge 53 vya methamphetamine, zaidi ya mifuko 200 ya plastiki inayodaiwa kutumika kufungashia dawa za kulevya pamoja na simu ya mkononi.

Kwa mujibu wa polisi, walikuwa wakimshuku Mekha kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya lakini wakaamua kutumia mbinu ya kujificha kama wacheza shoo kwenye tamasha hilo ili asishtuke na kutoroka.

Ripoti mbalimbali zimeeleza kuwa operesheni hiyo ilifanikiwa baada ya maafisa hao kuchanganyika na watu waliokuwa wakisherehekea kwenye tamasha hilo kabla ya kumzingira na kumkamata mshukiwa huyo ghafla.

Baada ya picha za operesheni hiyo kusambaa mtandaoni, watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii walitoa maoni tofauti huku baadhi wakilinganisha tukio hilo na filamu maarufu ya polisi ya “21 Jump Street”.

Kwa sasa Mekha anashikiliwa na polisi akisubiri hatua zaidi za kisheria.

...See more

WEKA COMMENT YAKO HAPA(MAONI)KUHUSU MADA HII

Related Discussions...