PSG Yatwaa Tena Taji la Ligi ya Mabingwa Baada ya Kuizamisha Arsenal kwa Penalti
Klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) imeendelea kuthibitisha ubabe wake barani Ulaya baada ya kutwaa taji la UEFA Ligi ya Mabingwa kwa mara ya pili mfululizo, ikiiadhibu Arsenal kwa mikwaju ya penalti 4-3 katika fainali yenye ushindani mkubwa iliyopigwa jijini Budapest.
Mchezo huo uliokuwa na kila aina ya hisia ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 baada ya dakika 120 za kawaida na za nyongeza, kabla ya mshindi kupatikana kupitia mikwaju ya penalti.
Arsenal waliingia uwanjani kwa ari kubwa na kuonyesha dhamira ya kutwaa taji hilo mapema kabisa. Dakika ya sita pekee ilitosha kwa Kai Havertz kuwainua mashabiki wa Gunners baada ya kufunga bao la kuongoza kufuatia hitilafu ya safu ya ulinzi ya PSG. Bao hilo liliwapa Arsenal mwanzo mzuri na matumaini ya kuandika historia mpya katika soka la Ulaya.
Katika kipindi kikubwa cha mchezo huo, Arsenal walionekana kuwa na mpangilio mzuri wa kujilinda. Beki Gabriel Magalhães alikuwa miongoni mwa nyota wa mchezo kwa upande wa Arsenal, akionyesha uwezo mkubwa wa kuzuia mashambulizi ya PSG na kuongoza safu ya ulinzi kwa utulivu mkubwa.
Hata hivyo, PSG walibadilika kabisa kipindi cha pili na kuanza kulisakama lango la Arsenal kwa mashambulizi ya mara kwa mara. Juhudi zao zilizaa matunda walipopata penalti baada ya Kvicha Kvaratskhelia kuangushwa ndani ya eneo la hatari. Ousmane Dembélé alisimama nyuma ya mpira na kufunga kwa utulivu, akiisawazishia PSG bao muhimu lililorejesha matumaini ya kutwaa ubingwa.
Baada ya sare hiyo kudumu hadi mwisho wa muda wa nyongeza, timu hizo zilielekea kwenye mikwaju ya penalti. Kipa David Raya aliipa Arsenal matumaini kwa kuokoa penalti moja ya PSG, lakini presha ya hatua hiyo ikaonekana kuwa kubwa kwa baadhi ya wachezaji.
Mkwaju wa mwisho wa Gabriel ndio uliogeuka kuwa tukio la kusikitisha kwa Arsenal. Penalti yake ilipaa juu ya lango na kuiacha PSG ikisherehekea ushindi mkubwa mbele ya maelfu ya mashabiki waliokuwa wamefurika uwanjani.
Kwa ushindi huo, PSG wameongeza ukurasa mwingine wa mafanikio katika historia yao ya soka la Ulaya, huku Arsenal wakilazimika kusubiri tena ndoto yao ya kutwaa taji la kwanza la UEFA Champions League. Matokeo hayo pia yameongeza majonzi kwa mashabiki wa Arsenal ambao bado wanakumbuka kupoteza fainali ya mwaka 2006 dhidi ya Barcelona.
Kwa upande wa PSG, ushindi huo unaimarisha hadhi yao kama moja ya klabu zenye nguvu zaidi barani Ulaya katika miaka ya karibuni, wakionyesha uthabiti, uzoefu na uwezo mkubwa wa kushinda mechi muhimu chini ya presha kubwa.



Post a Comment