Rais wa Marekani, Donald Trump, amewasili rasmi mjini Beijing nchini China kwa ziara Maalum
Rais wa Marekani, Donald Trump, amewasili rasmi mjini Beijing nchini China kwa ziara yenye uzito mkubwa kisiasa na kiuchumi, huku akipokelewa kwa heshima kubwa na viongozi waandamizi wa China kabla ya mazungumzo muhimu na Rais Xi Jinping.
Trump alishuka kwenye ndege ya Air Force One Jumatano jioni na kupokewa na Makamu wa Rais wa China, Han Zheng, jambo ambalo wachambuzi wengi wa siasa za kimataifa wamelitafsiri kama ishara ya heshima maalum kutoka Beijing kwa kiongozi huyo wa Marekani.
Ziara hiyo ya siku mbili inatarajiwa kugusa masuala nyeti yanayoathiri dunia kwa sasa, ikiwemo vita ya ushuru wa biashara kati ya Marekani na China, ushindani wa teknolojia, mvutano kuhusu Taiwan pamoja na vita vinavyoendelea kati ya Marekani, Israel na Iran ambavyo vimeendelea kuyumbisha uchumi wa dunia.
Trump anarudi China katika kipindi ambacho taifa hilo limeonekana kuwa na ushawishi mkubwa zaidi kimataifa ukilinganisha na ziara yake ya mwisho mwaka 2017. Wakati huo huo, rais huyo anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa jamii ya kimataifa kuhusu kampeni ya kijeshi ya Marekani katika Mashariki ya Kati.
Awali ziara hiyo ilikuwa imepangwa kufanyika mwezi Machi, lakini ikaahirishwa kutokana na kuongezeka kwa vita kati ya Marekani, Israel na Iran. Mvutano huo umeendelea kuathiri bei za mafuta, biashara za kimataifa pamoja na hali ya uchumi duniani.
Mkutano wa Trump na Xi Jinping unatazamwa kwa karibu na mataifa mengi duniani kutokana na nafasi kubwa ya Marekani na China katika uchumi wa kimataifa. Wachambuzi wanaamini kuwa mazungumzo hayo yanaweza kuathiri mwelekeo wa biashara, teknolojia na siasa za dunia katika kipindi kijacho.
Kupokelewa kwa Trump na kiongozi mkubwa kama Han Zheng pia kumeibua mjadala, kwani katika ziara yake iliyopita alipokelewa na viongozi wa ngazi ya chini zaidi, hali inayotafsiriwa kuwa China imeamua kuonyesha ushirikiano na umuhimu wa mahusiano yake na Marekani licha ya tofauti zilizopo kati ya mataifa hayo mawili.





Post a Comment
Karibu Afyaclass Bongo Social,Share mawazo yako hapa au chochote kuhusiana na Makala husika,Karibu Sana Mdau Wetu Muhimu.