Urusi na Ukraine Zinakaribia Mwisho wa Vita? Putin Azungumza Wakati wa Sitisho la Mapigano
Rais Vladimir Putin amesema vita kati ya Urusi na Ukraine vinaelekea kufikia mwisho, huku siku ya kwanza ya sitisho la mapigano lililosimamiwa na Marekani ikigubikwa na madai ya ukiukwaji kutoka pande zote mbili.
Putin alitoa kauli hiyo Jumamosi baada ya kuhudhuria gwaride la Siku ya Ushindi mjini Moscow, ambapo aliendelea kutetea operesheni ya kijeshi ya Kremlin nchini Ukraine na kuikosoa nchi za Magharibi kwa kuendelea kuiunga mkono Kyiv.
Akizungumza mbele ya wanajeshi waliohudhuria hafla hiyo, Putin alisema Urusi inapambana na “nguvu ya uchokozi” inayoungwa mkono na NATO, huku akisisitiza kuwa malengo ya Urusi katika vita hivyo bado yana msingi wa haki.
Alisema nchi za Magharibi zilianza kuongeza mvutano dhidi ya Urusi na zinaendelea kufanya hivyo hadi sasa, lakini akaongeza kuwa anaamini vita hivyo vinaelekea mwisho ingawa bado ni suala zito.
Putin pia alisema mataifa ya Magharibi yalitarajia Urusi ingeshindwa vibaya na mfumo wake wa dola kuporomoka kutokana na vita hivyo, lakini matarajio hayo hayakutimia.
Kauli hizo zimekuja wakati Urusi na Ukraine zikishutumiana kwa kukiuka sitisho la mapigano la siku tatu lililotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump. Licha ya tuhuma hizo, hakukuwa na mashambulizi makubwa ya makombora yaliyoripotiwa katika siku ya kwanza ya makubaliano hayo, ingawa mashambulizi ya droni na vifo vya raia viliripotiwa kutoka pande zote.
Trump alisema sitisho hilo linaweza kuwa mwanzo wa mwisho wa vita hivyo vya muda mrefu vilivyosababisha vifo vingi na uharibifu mkubwa.
Aidha, Trump alisema makubaliano hayo yanajumuisha mpango wa kubadilishana wafungwa kati ya Urusi na Ukraine. Ripoti zinaeleza kuwa kila upande unatarajiwa kubadilishana wafungwa 1,000.
Hata hivyo, Kremlin imesema kwa sasa hakuna mpango wa kuongeza muda wa sitisho hilo baada ya kipindi kilichokubaliwa kuisha.
Putin pia alisema yuko tayari kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy katika nchi ya tatu, lakini tu baada ya masharti yote ya makubaliano ya amani kukamilishwa kwanza.

.jpeg)



Post a Comment
"Karibu kutoa maoni yako. Kumbuka: Link zote za matangazo haziruhusiwi na zitafutwa kiotomatiki".