Serikali ya Marekani Yapanga Kuchapisha Noti ya Dola 250 Yenye Picha ya Trump
Serikali ya Marekani kupitia Idara ya Hazina imeanza maandalizi ya uwezekano wa kuchapisha noti mpya ya dola 250 yenye picha ya Rais Donald Trump, hatua ambayo imezua mjadala mkubwa nchini humo.
Kwa sasa sheria za Marekani haziruhusu rais aliye hai kuwekwa kwenye sarafu au noti za taifa hilo. Hata hivyo, maafisa wa utawala wa Trump wamesema wanafanya maandalizi mapema iwapo Bunge la Marekani litapitisha sheria maalum kuruhusu noti hiyo mpya.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Ikulu ya White House, Waziri wa Hazina Scott Bessent alisema suala hilo sasa liko mikononi mwa wabunge wa Capitol Hill.
“Tumefanya maandalizi ya awali, lakini tutaendelea kuheshimu sheria zilizopo,” alisema Bessent.
Aliongeza kuwa haoni tatizo lolote kwa rais ambaye alikuwa madarakani wakati Marekani ikiadhimisha miaka 250 ya uhuru wake kuwekwa kwenye noti maalum ya kumbukumbu.
Wazo la noti hiyo lilianzishwa mwaka jana na mbunge wa Republican kutoka South Carolina, Joe Wilson, ambaye alipendekeza sheria itakayolazimisha Idara ya Hazina kuchapisha noti ya dola 250 yenye picha ya Trump. Hata hivyo, muswada huo bado haujajadiliwa rasmi bungeni.
Kwa mujibu wa gazeti la Washington Post, baadhi ya maafisa walioteuliwa kisiasa katika utawala wa Trump tayari walikuwa wameanza kuandaa michoro ya noti hiyo pamoja na sura ya rais huyo.
Iwapo sheria hiyo itapitishwa, Donald Trump atakuwa mtu wa kwanza aliye hai kuwekwa kwenye fedha ya Marekani tangu mwaka 1866.
Trump tayari ameweka historia nyingine mapema mwaka huu baada ya Idara ya Hazina kutangaza kuwa saini yake itaonekana kwenye fedha mpya zitakazochapishwa, tofauti na utaratibu wa zamani uliotumia saini za Waziri wa Hazina na Mweka Hazina wa Marekani.

.jpg)


Post a Comment