Serikali ya Zanzibar imewapiga marufuku wachinjaji wenye ugonjwa wa homa ya ini kushiriki shughuli za uchinjaji kuelekea sikukuu ya Eid al-Adha, katika hatua ya kuimarisha usalama wa afya kwa wananchi.

Hatua hiyo imetangazwa wakati ambapo zaidi ya wanyama 5,000 wanatarajiwa kuchinjwa visiwani humo kwa ajili ya maadhimisho ya Eid al-Adha. Kwa mujibu wa Daktari wa Mifugo kutoka Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Dk. Fatma Said, marufuku hiyo inalenga kuzuia maambukizi yanayoweza kusababishwa na uchinjaji usiozingatia kanuni za afya.

Akizungumza na Nipashe Digital, Dk. Fatma amesema jumla ya wanyama 5,026 wanatarajiwa kuchinjwa, wakiwemo ng’ombe 3,481, mbuzi 1,203 pamoja na kondoo 342. Amesema serikali tayari imekagua machinjio yote yatakayohusika katika shughuli hizo.

“Tumesisitiza wachinjaji wote kupima afya zao mapema, kwani mtu mwenye homa ya ini anaweza kusababisha maambukizi kwa watu wengine kupitia mazingira au nyama isiyoshughulikiwa kwa usalama,” amesema Dk. Fatma.

Aidha, amesema wataalamu wa mifugo watakuwepo katika maeneo yote ya machinjio wakati wa Eid ili kuhakikisha kila mnyama anakaguliwa kabla na baada ya kuchinjwa kwa lengo la kudhibiti magonjwa yanayoweza kuambukizwa kutoka kwa mifugo kwenda kwa binadamu.

Pia amewataka wachinjaji kuzingatia usafi wa mazingira, matumizi ya vifaa salama na kufuata maelekezo yote ya wataalamu wa mifugo ili kuhakikisha nyama inayotumiwa na wananchi inakuwa salama na yenye ubora unaohitajika.

Dk. Fatma amesisitiza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayekiuka taratibu za afya zilizowekwa, akieleza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha wananchi wanaadhimisha Eid al-Adha katika mazingira salama na yenye kulinda afya za jamii.

...See more

WEKA COMMENT YAKO HAPA(MAONI)KUHUSU MADA HII

Related Discussions...