Trump Akosoa Bei Kubwa za Tiketi za Kombe la Dunia 2026

Rais wa Marekani Donald Trump amesema hata yeye binafsi hawezi kulipa bei kubwa zinazotozwa kwa tiketi za Kombe la Dunia 2026, hatua inayozidi kuongeza mjadala kuhusu gharama za mashindano hayo makubwa yatakayofanyika Marekani, Canada na Mexico.

Trump alitoa kauli hiyo katika mahojiano na gazeti la New York Post baada ya kuulizwa kuhusu tiketi za mchezo wa ufunguzi wa timu ya Marekani dhidi ya Paraguay huko Los Angeles ambazo zimefikia dola 1,000 kwa tiketi ya kawaida kabisa.

“Ningependa kuwepo huko, lakini ukweli ni kwamba hata mimi nisingelipa kiasi hicho,” alisema Trump.

Kauli hiyo imeonekana kama pigo kwa rais wa FIFA Gianni Infantino ambaye hivi karibuni alikuwa akitetea bei hizo licha ya malalamiko makubwa kutoka kwa mashabiki wa soka duniani.

Trump aliendelea kueleza kuwa angependa kuona watu wa kawaida waliomuunga mkono wakipata nafasi ya kushuhudia mashindano hayo bila kubanwa na gharama kubwa.

“Ningesikitika kama watu wa Queens, Brooklyn na wale wote wanaompenda Donald Trump wasingeweza kwenda kushuhudia mechi hizo,” alisema.

Kwa upande wake, Infantino amekuwa akitetea mfumo wa bei za tiketi akidai kuwa hata kushuhudia michezo mingine ya Marekani kama michezo ya vyuo vikuu au ligi za kitaalamu kunahitaji fedha nyingi zaidi.

Hata hivyo, madai hayo yalipingwa haraka baada ya kubainika kuwa tiketi za mchezo wa baseball wa timu ya New York Yankees dhidi ya Texas Rangers zilikuwa zikiuzwa kwa dola 8 pekee siku hiyo hiyo.

Katika mkutano mwingine wa hivi karibuni, Infantino aliulizwa kuhusu tiketi ya fainali ya Kombe la Dunia iliyokuwa imeorodheshwa kwa dola milioni 2 kwenye soko la kuuza tiketi mtandaoni. Akijibu kwa utani alisema angeenda binafsi kumpatia mnunuzi “hot dog na soda” ili kuhakikisha anapata uzoefu mzuri kwenye mchezo huo utakaochezwa katika uwanja wa MetLife Stadium.

FIFA imeeleza kuwa zaidi ya watu milioni 500 wameomba tiketi za mashindano hayo, ingawa taarifa zinaonyesha kuwa baadhi ya bei zimeanza kushuka katika majukwaa ya kuuza tiketi kutokana na waandaaji kuendelea kuachia tiketi mpya kadri mashindano yanavyokaribia.

WEKA COMMENT HAPA(Reply)

"Karibu kutoa maoni yako. Kumbuka: Link zote za matangazo haziruhusiwi na zitafutwa kiotomatiki".