Uganda yakubali mpango wa Marekani wa kuwaweka Wamarekani karantini kufuatia mlipuko wa Ebola
Serikali ya Uganda imethibitisha kuwa imepokea ombi kutoka Marekani la kuanzisha kituo maalumu cha karantini na matibabu kwa Wamarekani watakaobainika kuwa wameambukizwa virusi vya Ebola kufuatia kuongezeka kwa hofu ya kuenea kwa ugonjwa huo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Akizungumza na BBC, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Uganda, Dkt Diana Atwine, amesema Uganda iko tayari kushirikiana katika mpango huo kutokana na uzoefu mkubwa wa nchi hiyo katika kupambana na milipuko ya Ebola kwa miaka kadhaa.
“Ndiyo, walitufikia kuhusu kuanzisha kituo cha Ebola hapa. Tuko wazi kwa hilo. Tuna utaalamu mkubwa nchini,” alisema Dkt Atwine.
Kauli hiyo imekuja wakati Uganda ikiendelea kuimarisha udhibiti katika mipaka yake kufuatia taarifa za watu wanaoshukiwa kuwa na Ebola kujaribu kuvuka kutoka maeneo yaliyoathirika zaidi mashariki mwa DRC.
Kwa mujibu wa Dkt Atwine, wagonjwa hao walikuwa wakielekea Uganda wakiamini kuwa wanaweza kupata matibabu bora na nafasi kubwa ya kupona.
“Siku tatu zilizopita tuliona wagonjwa wakijaribu kuvuka na kuingia nchini mwetu. Wana ndugu hapa ambao wamekuwa wakiwaambia kuwa wakifika Uganda watapata matibabu na kupona,” alisema.
Ameongeza kuwa baadhi ya watu hao tayari walikuwa na dalili kali za Ebola na walikiri kupoteza ndugu zao kutokana na ugonjwa huo.
“Walikuwa wanatoka katika maeneo yaliyo kitovu cha mlipuko, walikuwa na dalili kubwa za Ebola na pia walikuwa wakikiri kuwa wamepoteza baadhi ya ndugu zao,” aliongeza.
Kutokana na hali hiyo, Uganda imeeleza kuwa kuendelea kuacha mipaka wazi kunaweza kuongeza hatari ya kusambaa kwa maambukizi hayo nchini humo.
“Tuligundua kuwa tukiendelea kuweka mipaka wazi hatutaweza kuudhibiti mlipuko huu,” alisema Dkt Atwine.
Serikali ya Uganda pia imesema inashirikiana kwa karibu na DRC kuanzisha vituo vya upimaji na matibabu karibu na maeneo ya mpakani ili kusaidia watu wanaohitaji huduma za afya bila kulazimika kuvuka mipaka.
“Tunafanya kazi pia na DRC kuanzisha vituo vya upimaji na matibabu upande wa mpakani kwa watu wanaotafuta huduma za afya na wanaojaribu kuvuka mpaka,” alisema.
Hatua hizi zinachukuliwa wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likiendelea kutoa tahadhari kuhusu umuhimu wa kudhibiti mlipuko huo haraka ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo katika mataifa ya Afrika ya Kati na Mashariki.





Post a Comment
Related Discussions...