Ugonjwa wa Ebola ni ugonjwa hatari unaosababishwa na virusi vya Ebola.
Ugonjwa wa Ebola husababishwa na Virusi ambao wanapatikana kwenye genus ya Orthoebolavirus ndani ya famili ya filoviridae. Aina sita za Orthoebolavirus zimetambuliwa hadi sasa, huku tatu zikijulikana kusababisha milipuko mikubwa:
- Ebola virus (EBOV) causing Ebola virus disease (EVD)
- Sudan virus (SUDV) causing Sudan virus disease (SVD)
- Bundibugyo virus (BDBV) causing Bundibugyo virus disease (BVD).
Ugonjwa huu huathiri binadamu pamoja na baadhi ya wanyama kama nyani na sokwe. Ebola huenea kwa kasi kupitia kugusana moja kwa moja na damu, mate, jasho, matapishi, mkojo au majimaji mengine ya mwili wa mtu aliyeambukizwa.
Historia ya Ebola ilianza mwaka 1976 ambapo milipuko miwili iligunduliwa kwa wakati mmoja nchini Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Ugonjwa huo ulipewa jina la Ebola kutokana na Mto Ebola uliopo karibu na eneo ambalo mlipuko mkubwa ulitokea nchini Congo.
Kwa mujibu wa World Health Organization, kuna aina mbalimbali za virusi vya Ebola lakini tatu ndizo zimekuwa zikisababisha milipuko mikubwa zaidi duniani. Ugonjwa huu una kiwango kikubwa cha vifo ambapo wastani wa vifo unaweza kufikia asilimia 50, na wakati mwingine kufika hadi asilimia 90 kutegemea aina ya virusi na huduma ya matibabu inayopatikana.
Chanzo kikuu cha Ebola kinaaminika kuwa ni popo wa porini wanaokula matunda. Binadamu wanaweza kupata maambukizi kupitia kugusa au kula wanyama walioambukizwa kama sokwe, nyani au popo. Baada ya mtu mmoja kuambukizwa, ugonjwa unaweza kuenea kutoka mtu hadi mtu kupitia majimaji ya mwili au vitu vilivyochafuliwa kama nguo na mashuka.
Dalili za Ebola huanza kuonekana kati ya siku 2 hadi 21 baada ya maambukizi. Mwanzoni mgonjwa anaweza kupata:
- Homa kali
- Maumivu ya kichwa
- Uchovu mkubwa
- Maumivu ya misuli na viungo
- Koo kuwasha au kuuma
Baadaye dalili huwa kali zaidi na zinaweza kujumuisha:
• Kutapika
• Kuharisha
• Maumivu ya tumbo
• Upele mwilini
• Kushindwa kufanya kazi vizuri kwa figo na ini
• Kutokwa damu puani, mdomoni au kwenye haja kwa baadhi ya wagonjwa.
Madaktari huthibitisha Ebola kwa vipimo vya maabara kwa sababu dalili zake zinaweza kufanana na malaria, homa ya matumbo au magonjwa mengine ya kuambukiza.
Kuhusu tiba, hadi sasa hakuna dawa moja ya kawaida inayoponya aina zote za Ebola, lakini matibabu ya haraka huongeza nafasi ya kupona. Wagonjwa hupewa maji ya kutosha mwilini, dawa za kupunguza dalili na huduma maalumu hospitalini. WHO inapendekeza matumizi ya dawa maalumu za kingamwili kwa baadhi ya aina za Ebola kama ansuvimab na Inmazeb.
Pia kuna chanjo zilizothibitishwa kusaidia kupambana na baadhi ya aina za Ebola, ikiwemo chanjo ya Ervebo. Chanjo hizi hutumika hasa wakati wa milipuko ili kuzuia maambukizi zaidi.
Milipuko mikubwa ya Ebola iliyowahi kutokea ni pamoja na ule wa Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 hadi 2016 ambapo maelfu ya watu walifariki katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone. Huo ulikuwa mlipuko mkubwa zaidi kuwahi kurekodiwa tangu ugonjwa huo ugunduliwe.
Kwa sasa mashirika ya afya duniani yanaendelea kufuatilia milipuko mipya ya Ebola katika baadhi ya maeneo ya Afrika ya Kati, huku WHO ikisisitiza umuhimu wa uchunguzi wa haraka, kutenga wagonjwa, chanjo na elimu kwa jamii ili kuzuia maambukizi zaidi.
Vyanzo vikuu vya afya:
•https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/ebola-disease?





Post a Comment
Related Discussions...