Walinzi matatani,Kijana kuvuka vizuizi vya kiusalama na kumkumbatia rais Ruto

Jeshi la Polisi nchini Kenya limeanzisha uchunguzi maalumu kufuatia tukio la kijana mmoja kufanikiwa kupenya ulinzi wa Rais wa Kenya, William Ruto, wakati wa hafla ya hadhara iliyofanyika eneo la Ganze, Kaunti ya Kilifi Mei 24, 2026.

Tukio hilo lilitokea wakati Rais Ruto alipokuwa akizungumza katika hafla ya kumpongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana, Fikirini Jacobs, ambapo kijana huyo alivuka vizuizi vya kiusalama akiwa ameshika Biblia na kufanikiwa kumfikia pamoja na kumkumbatia rais mbele ya mamia ya wananchi waliohudhuria.

Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi Kenya, mamlaka zilisema tukio hilo limechukuliwa kama uvunjifu mkubwa wa usalama wa taifa licha ya vikosi vya ulinzi kufanikiwa kudhibiti hali hiyo haraka bila madhara yoyote kutokea.

Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kirocho, amesema tayari ameunda timu maalumu ya uchunguzi ili kubaini namna kijana huyo alivyoingia hadi eneo la rais pamoja na kutathmini upya mifumo ya kiusalama inayotumiwa katika shughuli za viongozi wakuu wa taifa.

“Tukio lolote linalohusisha usalama wa mkuu wa nchi ni suala nyeti la usalama wa taifa na litashughulikiwa kwa uzito mkubwa,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo, wakati vyombo vya usalama vikichunguza tukio hilo kama tishio la kiusalama, taarifa zimeeleza kuwa kijana huyo baadaye alipewa nafasi ya kazi katika Mamlaka ya Bandari Kenya (KPA), jambo lililozua mjadala mkubwa miongoni mwa wananchi na kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na John Macharia, kijana huyo alisema aliamua kuvuka ulinzi akiwa na Biblia iliyokuwa imehifadhi wasifu wake wa kazi (CV), akieleza kuwa alikuwa ametafuta ajira kwa muda mrefu bila mafanikio.

“Nimekuwa nikitafuta kazi kwa muda mrefu na nikaona hii ndiyo nafasi pekee ya Rais kuniona na kunisaidia,” alinukuliwa kijana huyo akisema.

Katika hali iliyowashangaza wengi waliohudhuria hafla hiyo, Rais Ruto aliwaagiza walinzi wake kutomdhuru kijana huyo na badala yake wamsikilize kabla ya kumuahidi msaada.

“Huyu kijana ana ujasiri, tutamsaidia,” alisema Rais Ruto huku akishangiliwa na wananchi.

Tukio hilo limeendelea kuzua mjadala mkubwa nchini Kenya, ambapo baadhi ya wananchi wameisifu hatua ya rais kuonyesha huruma kwa kijana huyo, huku wengine wakieleza hofu kuhusu udhaifu wa mfumo wa ulinzi wa viongozi wa taifa.

...See more

WEKA COMMENT YAKO HAPA(MAONI)KUHUSU MADA HII

Related Discussions...