Wanaume Wachangia Zaidi Matatizo ya Ugumba Tanzania – MNH

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imesema kuwa wanaume sasa wanachangia kwa kiwango kikubwa matatizo ya ugumba miongoni mwa wanandoa wanaotafuta huduma za uzazi kwa njia ya upandikizaji wa mimba maabara (IVF).

Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa Uzazi na Magonjwa ya Wanawake pamoja na Mkuu wa Kitengo cha IVF na Endocrinolojia ya Uzazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Matilda Ngarina, takribani theluthi mbili ya wanaume wanaofika kupata ushauri wa huduma hizo hubainika kuwa na mbegu dhaifu ambazo haziwezi kurutubisha mayai na kusababisha ujauzito.

Akizungumza kuhusu mwenendo wa huduma za IVF tangu zilipoanzishwa hospitalini hapo mwaka 2024, Dk. Ngarina alisema mtazamo wa zamani uliokuwa ukiwahusisha wanawake pekee na matatizo ya uzazi sasa umeanza kubadilika, baada ya tafiti na uchunguzi kubaini kuwa wanaume pia ni chanzo kikubwa cha changamoto hizo.

Alieleza kuwa baadhi ya wanaume wanaofika hospitalini hapo hukutwa hawana mbegu kabisa, huku wengine wakiwa na kiwango kidogo cha mbegu au mbegu zisizokuwa na uwezo mzuri wa kutembea kuelekea kwenye yai kwa ajili ya urutubishaji.

“Baadhi ya wanaume hawana mbegu kabisa, wengine wana mbegu chache zisizotembea vizuri, huku wengine wakiwa na mbegu zenye hitilafu katika mkia na kichwa,” amesema Dk. Ngarina.

Huduma za IVF zimeendelea kuwa msaada mkubwa kwa wanandoa wanaopitia changamoto za kupata watoto, huku wataalamu wakisisitiza umuhimu wa wenza wote wawili kufanya uchunguzi mapema badala ya kumtupia lawama mwanamke pekee.

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa sababu mbalimbali zinaweza kuathiri ubora wa mbegu za kiume, ikiwemo matumizi ya pombe kupita kiasi, uvutaji sigara, msongo wa mawazo, lishe duni, magonjwa ya mfumo wa uzazi pamoja na mtindo wa maisha usiozingatia afya.

Kuongezeka kwa uelewa kuhusu afya ya uzazi kwa wanaume kunatajwa kuwa hatua muhimu katika kupunguza changamoto za ugumba nchini, huku huduma za kisasa kama IVF zikitoa matumaini kwa familia nyingi zinazotamani kupata watoto.

...See more

DISCUSSIONS BOX(MAONI)|REPLY

Related Discussions...